Gamondi: Tumejiandaa kukabiliana na Mamelodi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Yanga itavaana na Mamelodi kesho saa 3:00 usiku, mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema ili timu hiyo ifikie mafanikio ya juu lazima icheze dhidi ya klabu kubwa za Afrika kama Mamelodi Sundowns.

Yanga itavaana na Mamelodi kesho saa 3:00 usiku, mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Gamondi amesema timu yake imejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo muhimu zaidi kwao.

"Kila mtu anajua Mamelodi ni klabu bora Afrika, lakini tumejiandaa kupambana na kila klabu mbele yetu. Ukweli, mechi hii imekuja kipindi ambacho kuna mapumziko ya mechi za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na kimsingi kwa namna moja inaweza kuathiri maandalizi yetu, lakini tupo kamili.

"Unapohitaji kufika madaraja ya juu ya soka la Afrika, lazima ucheze dhidi ya miamba. Mechi hii ya Mamelodi ni changamoto nzuri sana. Kwangu huu umekuwa msimu mzuri, tumecheza na Al Ahly na sasa Mamelodi," alisema Gamondi ambaye aliwahi kuifundisha Mamelodi.

Baada ya mchezo huu, timu hizo zitarudiana wikiendi ijayo Afrika Kusini na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali.