Gamondi: Pacome, Aucho hawachezi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema hajawaona mastaa wake wawili kambini Stephane Aziz KI na Djigui Diarra lakini amekiandaa kikosi chake kuhakikisha kinaonyesha ushindani.

Yanga itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Jumamosi kuanzia saa 3:00 usiku dhidi ya Mamelodi Sundowns mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gamondi amesema nyota hao waliokuwa na vikosi vya timu zao za taifa kwa michezo ya kirafiki Aziz KI akiwa na Burkina Fasa na Diarra akiwa na Mali na ameambiwa wamerudi leo asubuhi ingawa bado hajawaona. Pia amesema ana wachezaji majeruhi zaidi ya watatu na kukiri anaweza akawakosa katika mchezo huo.

"Ukiachana na kina Aziz KI na Diarra ambao watakuja kesho asubuhi, pia nina baadhi ya wachezaji ambao wana shida ya majeraha, Kouassi Yao, Pacome Zouzoua, Kibwana Shomari na Khalid Aucho hivyo hiki kitu kinanichanganya kwenye mbinu zangu," amesema na kuongeza;

"Mimi kama kocha natakiwa kuwa na mbinu mbadala na kuandaa kikosi ambacho kitanipa matokeo, nawaomba mashabiki kujitokeze kwa wingi kutupa sapoti kwa ajili ya mchezo wetu wa kesho," amesema.

Kuhusu maandalizi kwa jumla, Gamondi amesema kwake hayakuwa mazuri kutokana na kutokuwa na wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza, hata hivyo hilo halitawazuia kucheza kama walivyozoea.

Gamondi anasema kuna michezo miwili sio kesho pekee, hivyo anapambana kuhakikisha anawajenga wachezaji wake kisaikolojia ili wacheze kwa kuhakikisha wanatoa furaha kwa mashabiki wao.

"Kwetu ni changamoto nzuri kukutana na timu kama Mamelodi na Yanga, ni timu ambayo imeshiriki michuano hiyo kwa miaka mingi imeshakutana na Al Ahly na sasa inakutana na mpinzani huyo mpya," amesema Gamondi.

Amesema amewaandaa wachezaji wake kucheza mpira kwa kushirikiana na kuhakikisha hawafanyi makosa kwa sababu wanakutana na timu ambayo ina uzoefu mkubwa kwenye michuano hiyo.

Kocha wa Mamelodi, Rulani Mokwena amesema hawaogopi Yanga, anawaheshimu huku akikiri anachokiogopa ni kifo tu.

"Kusema nawaogopa Yanga hapana, sio kweli bali nawaheshimu Yanga kitu pekee ambacho nakiogopa ni kifo lakini sio kuwaogopa Yanga," amesema Mokwena.