Gamondi: Kwa Uwanja ule unashindaje?

Muktasari:

  • Gamondi amesema Yanga kupata pointi moja kwenye uwanja mbovu kama ule sio kitu kibaya, ingawa hana furaha na maamuzi yaliyowafanya kucheza hapo.

BAADA ya kupata sare isiyo na mabao dhidi ya JKT Tanzania, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameshangaa maamuzi ya kulazimisha mchezo huo wa Lifi Kuu  ara kuchezwa kwenye Uwanja uliokosa ubora.

Yanga imepata sare ya pili ikicheza ugenini kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam ikiendelea kusalia kileleni ikifikisha pointi  59 baada ya kucheza mechi 23.

Gamondi amesema Yanga kupata pointi moja kwenye uwanja mbovu kama ule sio kitu kibaya, ingawa hana furaha na maamuzi yaliyowafanya kucheza hapo.

Kocha huyo raia wa Argentina, amesema uwanja kama huo unaharibu heshima ya Tanzania wakati soka la nchi likiendelea kupiga hatua.

"Kupata alama moja kwenye Uwanja kama ule ni kitu kizuri tu kwangu, unawezaje kushinda kwenye uwanja kama ule? Sijui ni maamuzi gani haya yamefanyika," amelalamika Gamondi.

"Huwezi kucheza mpira wa kuvutia kwenye Uwanja kama ule, tunaona soka la Tanzania linapiga hatua ni jambo zuri, lakini Uwanja kama huu unakwenda kuiweka wapi heshima hiyo, kwanini ilazimishwe mechi kuchezwa pale ingekuwa sawa hata kusogeza mechi mbele au kuhamishwa kupelekwa Uwanja mwingine," amesema Gamondi ambaye sare ya jioni ya leo ni ya pili kwa timu hiyo.

Aidha Gamondi amesema uwanja kama ule ni hatari hata kwa wachezaji ambapo anashukuru kwa kikosi chake hakuna taarifa mbaya ya kuumia kwa nyota wa timu hiyo.

Mchezo wa JKT dhidi ya Yanga ambao awali ilikuwa uchezwe jana Aprili 22 ulilazimika kusogezwa mbele baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam kujaza maji baadhi ya maeneo ya uwanja huo na kuamua kusogezwa mbele hadi leo.

Hata hivyo, baada ya vikao virefu vya juzi usiku Mwanaspoti linafahamu kuwa hesabu za kwanza baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo ilikuwa mechi hiyo ipelekwe Uwanja wa Azam Complex lakini uamuzi huo ukagomewa na timu wenyeji wakidai Uwanja huo utakuwa sawa kwa mchezo kuchezwa leo endapo mvua hazitaendelea.