Prime
Gamondi ayataja mabao matano

Muktasari:
- Watetezi hao walipata ushindi huo kwa bao la dakika ya 88 lililofungwa na, Mudathir Yahya kwenye mechi kali iliyopigwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi tisa na mabao 11 katika michezo mitatu iliyocheza hadi sasa ikiing’oa Mashujaa yenye pointi 7.
YANGA imepata ushindi mwembamba wa kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ikiifunga Namungo kwa bao 1-0 na kurejea kileleni mwa msimamo, lakini kocha wake, Miguel Gamondi akawatega wapinzani huku akitaja mabao matano.
Watetezi hao walipata ushindi huo kwa bao la dakika ya 88 lililofungwa na, Mudathir Yahya kwenye mechi kali iliyopigwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi tisa na mabao 11 katika michezo mitatu iliyocheza hadi sasa ikiing’oa Mashujaa yenye pointi 7.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Gamondi alisema timu hiyo imepata ushindi mdogo inatokana na mbinu za timu pinzani iliyoamua kuweka wachezaji wengi nyuma na kucheza mfumo wa kujilinda zaidi ambao uliwapa wakati mgumu kukamilisha mashambulizi yao.
Gamondi aliwatega wapinzani akisema, anafurahia ushindani ambao kikosi chake unaupata lakini akazitaka timu pinzani kuja na akili ya kuwashambuliana na sio kubaki nyuma muda mwingi.
“Ilikuwa vigumu kufanya mambo kama ambavyo tunataka, tumeinadaa timu yetu kushindana lakini unapocheza na timu inayokaa nyuma wakati mwingine ni vigumu kuona ubora,” alisema Gamondi aliyevuna mabao 22 na kuruhusu moja tu katika mechi nane za mashindano yote hadi sasa.
“Tuna timu inayocheza tumejiandaa kukutana na upinzani, lakini ni vizuri tukaona timu pinzani nazo zikitushambulia ili tushindane, haikuwa hivyo, jambo zuri tuliamua kubadilika na kutumia njia za pembeni kutafuta ushindi ambayo ilitusaidia na kufanikiwa,” aliongeza kocha huyo raia wa Argentina.
Kauli ya Gamondi imekuja kufuatia mbinu za Namungo ambayo ilikuwa inacheza mfumo wa 3-5-2 ulioifanya kuwa wengi nyuma ya mpira na kuwapa Yanga wakati mgumu kupenya ukuta wa wapinzani wao.
Aidha Gamondi aliwashusha presha mashabiki wa timu hiyo, akisema sio kila wakati watakuwa na ushindi wa mabao matano kama ambavyo walishinda mechi zilizopita lakini kitu muhimu ni ushindi.
“Mashabiki wetu hawaji uwanjani wakiwa na matarajio ya kushinda mabao matano kwa kila mchezo, ni lazima tuwe wakweli, wao wanakuja uwanjani wakiwa na matarajio ya kuona timu yao inashinda na hiki ndicho tutaendelea kukipigania, nakubali ni kiu yetu kuona tunashinda kwa mabao mengi,” alisema Gamondi anayehamishia nguvu sasa katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Merrikh ya Sudan, huku akiwa na mtaji wa ushindi wa mabao 2-0 alioupata ugenini jijini Kigali, Rwanda katika mechi ya awali.