Polisi yarejea Ligi Kuu Zanzibar

Muktasari:
- Timu ya Polisi iliyoshuka daraja msimu uliopita imerejea katika Ligi Kuu Zanzibar baada ya kuichakaza Kundemba mabao 3-1.
Licha ya vita vya ngumi na midomo iliyotokea leo Jumapili katika mechi ya jasho na damu, maafande wa Polisi wameichakaza Kundemba kwa kuitandika mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mao B, Mjini Unguja na msimu ujao watacheza Ligi Kuu Zanzibar.
Timu nyingine zilizotinga ZPL kwa msimu ujao ni; New King, Fufuni na Wawi.
Mechi hiyo iliyokuwa na hekaheka kwa mashabiki wa pande zote mbili kwa utani wa ngumi zilizopigwa uwanjani ilikuwa ya aina yake kwa wapenzi wa soka la Zanzibar.
Katika pambano hilo la marudiano ya mtoano, Kundemba ilionyesha kuutawala vyema dakika za mwanzo na kujipatia bao la mapema kabla ya kugeuziwa kibao.
Kipindi cha kwaza kilimaliza Kundemba wakiongoza bao1-0, jambo ambalo liliwafanya mashabiki wa Polisi kuonekana kukata tamaa na baadhi yao kuondoka uwanjani.
Bao hilo liliwatia hasira Polisi na kurejesha bao ambalo liliongeza kasi kuutawala mchezo na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, dakika 90 ziliiamua kwa timu ya Polisi kurudi tena ZPL msimu ujao.
Baada ya mchezo huo kumalizika mashabiki wa Kundemba walihisi wameonewa na kutaka kumpiga mwamuzi jambo lilosababisha kutolewa uwanjani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa usalama wa Polisi.
Kwa upande wa mashabiki waliokuwa nje ya uwanja walijipanga pembeni na kuanza kurusha mawe na mchezo huo kuweka historia ya kumalizika kwa hekaheka na mikiki.
Polisi inahitimisha kuwa miongoni mwa timu nne zilizopanda daraja ikitanguliwa na New King kwa Kanda ya Unguja iliyoitoa Sebleni na Kanda Pembeni Wawi na Fufuni zimefanikiwa kutinga ZPL kwa mara ya kwanza.
Mbali na hayo, Polisi sasa itavaana na New King 'Wachoma Mahindi' kutafuta bingwa wa Kanda ya Unguja ili kupambana na mshindi wa Kanda ya Pemba ili kupata bingwa wa Daraja la kwanza.