Gamondi awagawa kina Pacome mazoezini

WAKATI Yanga ikiendelea kujinoa mazoezini ili kujiandaa na mechi dhidi ya Belouizdad ya Algeria, kocha wa kikosi hicho Miguel Gamondi amewagawanya wachezaji wake.

Iko hivi. Yanga jana ilikuwa na mechi dhidi ya Polisi Tanzania ikiwa ni hatua tatu ya michuano ya Kombe la ASFC.

Mechi hiyo ilimalizika kwa kuwatupa nje ya michuano wapinzani wao kwa kuwashushia kipigo cha mabao 5-0 na kuandika historia ya kufunga mabao hayo kwenye mechi saba za michuano tofauti msimu huu.

Leo wakiwa mazoezini wachezaji hao wamegawanywa na kocha, huku wale waliocheza jana wakifanya mazoezi ya tofauti na wengine.

Na wale ambao jana hawakucheza kabisa na walioingia kutokea benchi wakifanya mazoezi magumu zaidi.

Miongoni mwa wachezaji walioko kwenye kundi la mazoezi mepesi ni kiungo hatari anayeongoza kwa idadi ya mabao 10 mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Bara.

Katika kundi la mazoezi magumu, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli walihusika pia bila kumsahau Khalid Aucho.

Hii inaonyesha picha kuwa katika mechi hiyo ngumu ya Ligi ya Mabingwa, itakuwa na wachezaji wengi kutokea katika kundi la wanaocheza mazoezi magumu.

Unaweza kusema Gamondi jana alichezesha kikosi ambacho kwa asilimia kubwa hatakitumia dhidi ya Belouizdad.


Yanga itashuka dimbani siku ya Jumamosi kusaka pointi tatu muhimu za kuwafanya wasalie katika michuano hiyo ambapo wako nafasi ya tatu kundi D wakiwa na alama tano wakiongozwa na Al Ahly (pointi 6) na Belouizdad (pointi 5). Mkiani wapo Medeama wenye pointi 4.

Katika mechi iliyopita kule Algeria, Yanga ilitawala mchezo lakini ilikumbana na kipigo kizito cha mabao 3-0, jambo ambalo litawalazimu Wanajangwani kucheza tofauti sana na walivyocheza kule ambako Belouizdad ilikuwa ikifunga mabao kwa mashambulizi ya kushtukiza yaliyozaa matunda na kuivuruga Yanga mwanzo-mwisho.