Gamondi achekelea Aziz KI kubaki Yanga

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki

Muktasari:

  • Kauli hiyo ya Gamondi inakuja baada ya saa chache kupita tangu Aziz KI kuthibitisha kwamba ataendelea kusalia ndani ya kikosi hicho.

Licha ya kutokuwepo kwenye mazoezi ya leo, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kila mtuĀ  ndani ya timu hiyo amefurahishwa na taarifa ya Stephanie Aziz Ki kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Kauli hiyo ya Gamondi inakuja baada ya saa chache kupita tangu Aziz KI kuthibitisha kwamba ataendelea kusalia ndani ya kikosi hicho.

Azizi Ki amerejea nchini leo allfajiri akitokea mapumziko baada ya msimu uliopita kumalizika, ambapo pia mkataba wake ulimalizika mara baada ya msimu huo.

Gamondi amesema uamuzi wa Azizi Ki kusalia Yanga unathibitisha kwamba amechagua kubaki sehemu inayompa amani na anayoamini itampa mafanikio.

Kocha huyo raia wa Argentina amesema kiungo huyo aliyeibuka mfungaji bora wa msimu uliopita akiwa na mabao 21, mara baada ya mkataba wake kufikia mwisho anaamini alikutana na ofa nyingi kubwa, lakini ameamua kusalia Yanga.

"Wakati tunamalizia msimu nilizungumza naye akaniambia anatamani sana kubaki licha ya kwamba amepokea ofa nyingi kubwa, ana amani kuwa hapa," amesema Gamondi.

"Kuna wakati kwenye maisha unaweza kupuuza fedha nyingi na kuchagua kubaki sehemu ambayo unaamini kama utabaki utakuwa na furaha lakini kikubwa kama unaona utapata mafanikio makubwa.

"Mashabiki wamefurahi lakini hata sisi tunaofanya naye kazi tumefurahishwa na uamuzi wake. Huyu ni mmoja kati ya wachezaji bora ambaye amefanya makubwa hapa."

Yanga Leo imefanya mazoezi kwenye Fukwe za Coco, ikiendelea na ratiba ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.