Fountain Gate yatwaa ubingwa soka la vijana U17

Muktasari:
- Timu ambazo zimeshiriki ni Marsh, Maswa Warriors, Musoma Boys, Ziwani FC, Ziba Sekondari, Kagongwa City, Foissa, Dhujau SC, Kim Canteen, Mshani SC, Fountain Gate, Kigoma- Ujiji SC, Tanzania Prisons na TFF Center Academy.
Mwanza. Timu ya kituo cha Fountain Gate cha Dodoma imetwaa ubingwa wa mashindano ya soka la vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa wavulana ambayo yamehitimishwa leo jijini Mwanza.
Mashindano hayo ya kusaka vipaji katika umri mdogo kwaajili ya timu za taifa za vijana imeanza Desemba 6 na kuhitimishwa leo Desemba 13, 2023 katika Uwanja wa nyamagana jijini hapa yakishirikisha timu 14.
Fountain imetwaa ubingwa wa mashindano hayo ya kwanza kitaifa nchini, leo Desemba 13, 2023 kwenye mchezo wa fainali ambao imeibuka na ushindi wa penalti 3-2 dhidi ya Musoma Boys ya mkoani Mara baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mabingwa hao wameaunza vizuri mchezo wakitawala kipindi cha kwanza na kutengeza nafasi nyingi za mabao, ambapo wametangulia kupata bao mapema dakika ya 10 likifungwa na Erick Marco baada ya beki wa Musoma, Elia Musa kushindwa kutuliza mpira aliorudishiwa.
Baada ya bao hilo, Musoma Boys wamefanya mabadiliko ya wachezaji dakika ya 35 wakimtoa Daniel Ryoba na kumuingiza Antony Paschal, ambapo yamewarejesha mchezoni na kusawazisha bao hilo dakika ya 74 kupitia kwa Andrea Vicent na dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mratibu wa mashindano hayo, Joel Balisidya, amesema lengo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuandaa mashindano hayo limefanikiwa kwani wameona ushindani na vipaji vikubwa ambavyo viko tayari kuendelezwa kwa matumizi ya baadaye.
“Tumepata bingwa kwa utaratibu mzuri timu zimeonyesha ushindani na hata fainali ya leo haikuwa nyepesi. Lengo la mashindano lilikuwa kutafuta vipaji katika umri sahihi tunashukuru tumeviona timu yetu ya ufundi imeonana jana na vijana wote waliochaguliwa na kufanya mazoezi ya pamoja,” amesema Balisidya
Kocha wa Fountain Gate, Buya Kassim amesema kilichowabeba na kufanikiwa kupata ubingwa huo ni mikakati ya muda mrefu tangu wakiwa mkoani Dodoma ambapo walijipangia kufika fainali na imewasaidia kushinda mechi zao, huku akiwapongeza TFF kwa kutengeza jukwaa hilo kwa ajili ya vipaji vichanga kuonekana.