Fei: Nilimuagiza Ninja ahamishe vitu vyangu Yanga

Muktasari:

  • Wakati Fei Toto anaondoka Yanga kulikuwepo na tetesi kwamba kitendo cha Ninja kuondoa vitu vyake ni kama viliwakwaza baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, lakini kwa upande wa beki huyo, alijibu kutoona tatizo kumsaidia mchezaji mwenzake kuhamisha vitu vyake.

Baada ya beki wa kati wa Lubumbashi Sport ya DR Congo, Mtanzania Abdallah Shaibu 'Ninja' kuzungumzia kuhusika kuvihamisha vitu vya aliyekuwa kiungo wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' katika klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Jangwani, Fei kazungumzia hilo.

Wakati Fei Toto anaondoka Yanga kulikuwepo na tetesi kwamba kitendo cha Ninja kuondoa vitu vyake ni kama viliwakwaza baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, lakini kwa upande wa beki huyo, alijibu kutoona tatizo kumsaidia mchezaji mwenzake kuhamisha vitu vyake.
 
"Mchezaji kuondoka kwenye timu ni jambo la kawaida. Siamini kama hiyo ni sababu na wala sikuona ubaya kumsaidia Fei Toto kumpelekea nguo zake, hivyo ulikuwa ni uvumi na wala siyo kweli kwa sababu chumba nilichokuwa nakaa kabla sijaenda Dodoma Jiji alikabidhiwa Tuisila Kisinda," amesema Ninja.

Mwanaspoti lilimtafuta Fei Toto kujua upande wake nani alimuagiza aondoe vitu vyake Yanga, ambapo amemtaja Ninja ndiye alimuomba kufanya hivyo.

"Ninja baada ya kurejea Yanga akitokea Dodoma Jiji kwa mkopo alikuwa anakaa kwenye chumba nilichokuwa nakaa. Sikuona ubaya yeye kunihamishia nguo zangu, kwani hata mimi mtu akiniagiza naweza nikafanya hivyo," amesema.

"Nimekujibu kwa sababu Ninja amesema, vinginevyo ningekaa kimya, lakini sijui kama hayo mambo yana nafasi kwa sasa, maana maisha mengine yameendelea."