Fei: Kila mechi Ligi Kuu Bara ni fainali

Muktasari:
- Kiungo huyo ambaye alifunga mabao 19 msimu ulioisha akishika nafasi ya pili nyuma ya Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyeshinda kiatu cha ufungaji bora kwa kuweka kambani mabao 21, hadi sasa timu yake imecheza mechi sita, hajafunga, lakini ametoa asisti tatu.
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema msimu huu ni mgumu kila mchezo ni fainali hakuna timu ndogo.
Kiungo huyo ambaye alifunga mabao 19 msimu ulioisha akishika nafasi ya pili nyuma ya Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyeshinda kiatu cha ufungaji bora kwa kuweka kambani mabao 21, hadi sasa timu yake imecheza mechi sita, hajafunga, lakini ametoa asisti tatu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto amesema ligi ni ngumu na hakuna timu nyepesi, hivyo wanatakiwa kujipanga vizuri kwa kila mpinzani kwa sababu wamekutana na ugumu ambao hawakuutarajia.
"Msimu huu kila timu imefanya usajili mzuri ina wachezaji wenye uchu wa mafanikio, hivyo kila mchezo ni fainali mipango mizuri ndio inaamua matokeo baada ya dakika 90," amesema na kuongeza:
"Bado ni mapema sana kuzungumzia mambo ya kiatu lakini ikitokea nafasi nitawania muda na mechi zilizobaki zinaruhusu na kutoa nafasi kwa mimi kupambana."
Fei Toto amesema licha ya kutokuwa na matokeo mazuri kwenye mechi za mwanzo malengo ni yaleyale kufanya vizuri na kurudi kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
"Tuna kikosi kizuri na wachezaji ambao wana uwezo wa kutoa changamoto kwa timu pinzani. Ni suala la muda kupata matokeo mazuri ambayo yatatoa ushindani kwa timu pinzani. Ni suala la muda tu na malengo yetu ni yaleyale kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili mfululizo," amesema.
"Mipango mizuri ya benchi la ufundi na sisi wachezaji ndio italeta chachu hakuna kinachoshindikana kwasababu tunacheza wachezaji 11 uwanjani na hao ambao wamekuwa wakitwaa mataji na kufanya vizuri na wao wanakuwa 11 hivyo jitihada binafsi na benchi la ufundi ndio msingi."
Fei toto amehusika kwenye mabao matatu kwenye mchezo dhidi ya KMC timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 alitoa pasi tatu zilizozaa mabao.