Fainali Simba, Yanga Kigoma, TFF yakomba Sh12 milioni kwa adhabu

Friday July 30 2021
bilioni pic 1
By Mwandishi Wetu

BAADA ya Simba kubeba kombe la Azam Shirikisho 2020/21 mbele ya watani wao Yanga kwa kuwafunga bao 1-0 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma sasa timu zote zitaonja chungu ya faini iliyotokana na mechi hiyo.

Kamati ya mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia taarifa yao imesema imejiridhisha na kutoa adhabu kwa makosa mbalimbali

"Simba wamepigwa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la viongozi na mashabiki kukaidi maelekezo, walilazimisha kuingia Uwanjani na kupita kwa nguvu mlango usio Rasmi wakati wa zoezi maalum la kutembelea uwanja wa mazoezi na kusababisha uharibifu wa mali, vurugu," imeeleza taarifa hiyo

Pia, wametozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la viongozi wao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, viongozi wa Simba walitumia mlango wa vyumba vya kubadilishia nguo, wachezaji kuingia uwanjani wakiambatana na watu mbalimbali miongoni mwao wasiokuwa na tiketi za kuingia uwanjani kinyume na utaratibu

Wekundu hao wa Msimbazi wametozwa faini ya Sh500,000 kwa mashabiki wake kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu kwa kusababisha vurugu na askari wa uwanjani wakati wa mapumziko kwenye eneo la vyumba vya kuvalia kinyume na utaratibu.

Wakati timu ikikumbana na rungu hilo mchezaji Bernard Morrison amepigwa faini ya Sh3 milioni na kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kimaadlili, kinidhamu na udhalilishaji wakati akishangalia ushindi.

YANGA

Yanga wao kwanza wamepigwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani na Sh 500,000 kwa kosa la washabiki wake kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu kwa mwamuzi wa akiba wa mchezo wakati wa mapumziko kinyume na utaratibu.

Mbali na hiyo wame imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la viongozi wao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, walitumia mlango wa mashabiki jukwaa la Urusi kuingia uwanjani (pitch area) wakiambatana na watu mbalimbali miongoni mwao wasiokuwa na tiketi za kuingia Uwanjani kinyume na utaratibu.

Advertisement

Wanajangwani pia wametozwa faini yaSh500,000 kwa kosa la mashabiki wake kuwashambulia waamuzi wa mchezo huo kwa chupa za maji kwa nyakati tofauti wakati wa mchezo kinyume na utaratibu
Kubwa zaidi Yanga SC wametozwa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la viongozi na mashabiki wake kukaidi maelekezo, walilazimisha kuingia uwanjani na kupita kwa nguvu mlango usio rasmi wakati wa zoezi maalum la kutembelea uwanja wa mazoezi na kusababisha uharibifu wa mali.

Kamati hiyo imemfungia kiungo wa Yanga Mukoko Tonombe michezo mitatu ya timu yake na faini ya Sh500,000 kwa kosa la kumpiga mshambuliaji wa Simba SC John Bocco kiwiko.

bilioni pic

Kadhalika kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amepigwa faini ya Sh500,000 kwa kugoma kuhudhuria mkutano wa maandalizi ya mchezo na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa fainali ya kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma

Naye kipa wa Yanga Faruk Shikhalo amelimwa faini ya Sh500,000 kwa makusudi kukwepa kusalimiana na waamuzi na wachezaji wa timu ya Simba kwenye mchezo huo wa fainal

Advertisement