Faida 5 za Wiki ya Mwananchi

Muktasari:

  • Ni tukio linaloambatana na shughuli mbalimbali lakini kubwa zaidi siku ya kilele chake huwa na mchezo baina ya Yanga na timu inayoalikwa kutoka nje ya nchi ambao hufunga rasmi tamasha hilo.

Tamasha la Wiki ya Mwananchi hufanyika kila mwaka hapa Tanzania likiwa maalum kwa ajili ya kufungua msimu kwa klabu ya Yanga.

Ni tukio linaloambatana na shughuli mbalimbali lakini kubwa zaidi siku ya kilele chake huwa na mchezo baina ya Yanga na timu inayoalikwa kutoka nje ya nchi ambao hufunga rasmi tamasha hilo.

Mwaka huu, kilele cha Tamasha hilo kitakuwa ni Jumamosi, Julai 22 na kitafungwa kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya Yanga na Kaizer Chiefs itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Ni jambo lilisilo la bahati mbaya kwa Yanga kuwa na tamasha kama hilo na kuna faida nyingi ambazo klabu inazipata ziwe za kisoka na hata zile zisizo za kisoka.

Makala hii inaangaza faida tatu kubwa ambazo klabu ya Yanga inazipata kwa kufanya tamasha la Wiki ya Mwananchi kila mwaka.

Kiufundi
Mchezo ambao unafanyika siku ya kilele cha wiki ya Mwananchi unalipa fursa benchi la ufundi la kuona mapokeo ya kikosi kwa kile ambacho wamekipata katika maandalizi ya msimu mpya.

Unatoa mwanga wa wapi ambako timu imeimarika na maeneo gani yameonyesha udhaifu ili yaweze kurekebishwa ili msimu unapoanza, yasiweze kuwa na athari hasi kwenye timu.

Ni mechi ya kuonyesha ni kwa namna gani wachezaji wanazifanyia kazi mbinu za mwalimu lakini pia kiwango cha ufiti wao baada ya kipindi kigumu cha maandalizi.

Kwa upande mwingine mechi za kama hizo za siku ya kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi zinasaidia katika athari ya kisaikolojia kwa wachezaji kwa kufahamu ukubwa wa klabu yao na mahitaji yake katika msimu mpya.

Kijamii
Ni tamasha linalokutanisha kundi kubwa la mashabiki wa Yanga na wadau mbalimbali wa mpira wa miguu ambao hutoka maeneo tofauti ndani na nje ya nchi kuja kulishuhudia na kushiriki.

Mkusanyiko huo mkubwa unasaidia kujenga umoja na mshikamano klabuni lakini katika mchezo wa soka kiujumla jambo linalosaidia kuongezeka kwa hamasa kwa timu wakati ikikaribia kuanza msimu mpya.

Lakini pia linasaidia kujenga mahusiano baina ya watu ambayo yanaweza kufungua milango na fursa tofauti kwa watu baadhi ambayo kikawaida ni vigumu kutokea pasipo kusanyiko kama hilo.

Ikumbukwe kwamba tamasha hili huwa linaambatana na zoezi la uchangiaji damu hivyo  jamii inanufaika kwa kuwa na uhakika wa uwepo wa akiba ya kutosha ya damu katika hospitali mbalimbali na hivyo kupunguza vifo vitokanavyo na upungufu wa damu.

Pamoja na hayo, pia ni tamasha ambalo limekuwa likihusisha utoaji wa misaada kwa watu wenye uhitaji kama wajawazito, wazee, yatima na wengine.

Kiuchumi
Yanga inaingiza fedha kupitia udhamini wa kampuni au taasisi mbalimbali ambazo huingia nazo mikataba ya kuwa miongoni mwa wadhamini wa tukio hilo.

Pia, inavuna fedha kutokana na mauzo ya bidhaa tofauti zenye nembo ya klabu ambapo inakuwa rahisi kuuza kwa idadi kubwa kutokana na uwepo wa watu wengi ambao sio rahisi kuwaona katika mechi za kawaida.

Kuna makusanyo yatokanayo na viingilio vya milangoni kwani ni mechi ambayo huwa inavuta takribani watu 60,000 ambao wanafanya klabu iingize kiasi kikubwa cha fedha.

Kunufaika kwingine ni kwa kuongeza kipato cha mtu mmojammoja kutokana na shughuli mbalimbali za kibiashara na za utoaji huduma ambazo huwa zinafanyika ndani na nje ya uwanja.