England yaifuata Ubelgiji 16 bora ikiiua Panama mabao 6-1

Timu ya England imeibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 baada ya kuisambaratisha Panama bila huruma kwenye fainali za Kombe la Dunia mchezo uliopigwa leo Jumapili  katika Uwanja wa Nizhny Novgorod, Russia
Ushindi huo unaipandisha England kileleni kwenye msimamo wa Kundi G ikiwa pointi 6 sawa na Ubelgiji lakini wakiwa na tofauti ya mabao ya kufunga.
Kwenye kundi hilo, Panama na Tunisia zimejikuta zikianza kufungasha virago baada ya kupoteza michezo yake miwili  kila timu.
Katika michezo miwili, Panama imezalisha mabao 9 baada ya kupoteza mchezo mbele ya Ubelgiji iliyoibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kupokea kipigo cha mabao 6 leo.
Mabao ya England yaliwekwa wavuni na Harry Kane aliyefunga ‘hat trick’, John Stones (2) huku bao la tatu likiwekwa wavuni na Jesse Lingard.
Panama itakamilisha mchezo wake wa mwisho dhidi ya Tunisia Juni 28 wakati England itakamilisha mechi yake dhidi ya Ubelgiji tarehe hiyohiyo.
Mchezo wa jana usiku, Ubelgiji iliiadhibu Tunisia mabao 5-2 na kukata tiketi yake mapema ya kucheza hatua ya 16 bora.
 Kikosi cha kwanza England kiliongozwa na Pickford; Walker, Stones, Maguire;Trippier, Loftus-Cheek, Henderson, Lingard, Young, Raheem Sterling, pamoja na Harry Kane