Dube aigawa Simba, Yanga

PRINCE Dube ameendelea kuzivuruga Simba na Yanga. Mashabiki wa klabu hiyo wamegawanyika kwa sasa baada ya kuibuka kwa taarifa nyota huyo aliyeigomea Azam FC, anatamani kuichezea Yanga, huku uongozi ukiweka bayana Simba imetuma ofa ya kumsajili sambamba na Al Hilal.

Ipo hivi. Dube alianza kuhusishwa na Yanga mara baada ya kudaiwa kugoma kuambatana na timu kwa baadhi ya mechi za mikoani na kuonekana Kwa Mkapa wakati vijana wa Jangwani wakimgonga Mwarabu 4-0.

Dube aliibuka uwanjani hapo wakati Yanga ikiifumua CR Belouizdad katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikaelezwa ni mgomo wa kushinikiza kutaka aondoke Azam.

Akadaiwa kurudisha kila kitu cha klabu hiyo na kupeleka mezani Dola 200,000 (zaidi ya Sh500 milioni) ili kuilipa klabu kwa kuvunja mkataba uliosalia.

Hata hivyo, mabosi wa Azam uliibuka na kukanusha Dube amesaliwa na mkataba mfupi. Mabosi hao walisisitiza Azam ina mkataba na Dube hadi mwaka 2025, ila hawana noma kumwachia iwapo tu, jamaa atawalipa Dola 300,000 (zaidi ya Sh700 milioni).

Pia walienda mbali na kusema milango i wazi kwa klabu yoyote inayomhitaji mchezaji huyo, muhimu ni wao kwenda kuzungumza nao na kuwalipa kiasi wanachokihitaji kumwachia Dube.

Siku chache baadaye, Azam ilitoa taarifa imepokea ofa kutoka klabu mbili za Simba na Al Hilal ya Sudan kutaka kumsajili Prince Dube aliyewavuruga hivi karibuni.

Taarifa hizo, zilijibiwa na watu wa upande wa Dube, wakimkariri nyota huyo akisema hana mpango na ofa za klabu hizo, kwani anapotaka kucheza anapajua yeye na hawezi kulazimishwa pa kwenda.

Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa kutokuwepo kwa usahihi wa mahali gani nyota huyo aliyefunga mabao saba katika Ligi Kuu kwa msimu huu ataibukia, tayari ameshawagawa mashabiki wa klabu za Samba na Yanga.

Baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wakipiga chapuo kwa viongozi wao kumalizana mapema na Azam ili jamaa atue kikosini na kuliamsha kama alivyokuwa akifanya alipokuwa Chamazi.

Pia wapo wengine wanaomkataa na kutoa sababu kwa nini klabu hizo zinapaswa kuachana naye hata kama ni bonge la mchezaji.

Mwanaspoti limepokea maoni lukuki ya wasomaji wakitoa msimamo wao juu ya nyota huyo na kuhusishwa na klabu hizo wanazoshabikia na limeamua kuyachapa kuonyesha namna alivyowagawanya mashabiki wa Simba na Yanga wengine wakimtaka na wengine wakimkataa.

Hata hivyo, wale wanaomtaka atue wanaweka bayana, ujio wa Dube kwa Simba utasaidia kuimarisha eneo la mbele la timu hiyo kwani washambuliaji wa sasa Freddy Koublan na Pa Omar Jobe waliosajiliwa dirisha dogo ni kama wamefeli mapema kabla hata hawajamaliza mtihani.

Kwa wale wa Yanga wanasema mwamba huyo akitua ataenda kuvivaa na kuvimudu viatu vilivyoachwa klabuni na Fiston Mayele aliyepo Pyramids, kwani awali Hafiz Konkoni alichemka na hata waliopo sasa, Joseph Guede, Kennedy Musonda na Clement Mzize kiatu kimewapwaya mno.

Kwa aina ya vikosi vya Kocha Miguel Gamondi wa Yanga na Abdelhak Benchikha wa Simba, Dube anafiti vizuri tu, kwa rekodi alizonazo ndani ya misimu minne aliyoichezea Azam iliyomsajili kutoka Highlangers ya Zimbabwe inayohusishwa pia kumtaka kumrejesha kikosini.

Licha ya kumudu kucheza kama mshambuliaji namba mbili na wakati mwingine akitokea pembeni, lakini Dube ni mshambuliaji wa mwisho, hivyo kwa vikosi vyote vya Simba akipangwa na kuanza analiamsha kama kawaida na kuwapa raha mashabiki wa timu hizo kongwe nchini.

Kama Dube akitua Simba inawezekana Benchikha akaanza langoni na Ayoub Lakred, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Che Malone, Henock Inonga, Babacar Sarr, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, kisha akamtupa Dube asimame mbele na Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.

Kwa upande wa Yanga kama itafanikiwa kumvuta kikosini, basi Gamondi anaweza kulipanga jeshi upya kwa langoni kusimama, Diarra Djigui, Yao Kouassi, Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI.

Achana na hayo, ebu zisome meseji za wasomaji wa Mwanaspoti waliomjadili Dube kwa kutuma ujumbe wao katika namba 0658-376417 na ile ya 0773-732271;


MIMI natamani sana Dube aende Simba kwa sababu matatizo makubwa kwa miaka ya hivi karibuni ni eneo la ushambuliaji.

Mdau


MIMI naona Dube achague kwenda Yanga kwani ndio sehemu sahihi kwake.

40MC.KV.TZ


NAWASHAURI viongozi wa Azam waachane na Dube aende anakotaka kwani wakiendelea kumng’ang’ania atawasumbua tu.

Jackson Mwambene, Mbeya


DUME ni mzuri kwa soka analocheza, lakini Simba msihangaike naye, jamaa keshaonyesha mapenzi kwa Yanga. Atatusumbua.

Fadhil Kikoti, Lindi


DUBE kachoka kucheza ndondo, kwa sasa anataka kucheza mechi za kimataifa na siku moja kuwepo na Dube Day, mwacheni aje Yanga ale raha.

MD, TMK

SIMBA imlete Dube na kumwacha Freddy aende zake, kwani tangu atue kikosini hana maajabu yoyote kama ilivyo kwa Pa Omary Jobe.

Fanuel, Chugga


NAPENDEKEZA Dube aende Simba kutokana na uhitaji wa mshambuliaji anayeweza kufunga zaidi ya waliopo.

Yohana Willson, Iringa

ACHENI Dube aje jangwani kwa Wananchi, huko hawezi kupata kombe hata la maji ya kunywa.

Leo Mwang’ande, Njombe

NAONA soka linaendeshwa kihuni. Dube anazingua tu na hana sababu ya kulalamika kwani hakujua kilichoandikwa kwenye mkataba wakati anasaini?

Yohana, Makambako

AZAM FC wapunguze dau ili mchezaji aondoke akatafute changamoto nyingine.

Mdau

AZAM isiwe ngumu, ijaribu kukumbuka wakati wa Fei Toto ilikuwaje au na wao wanataka Mama Samia atoe kauli tena?

Mdau.


DUBE aangalie masilahi asiangalie mapenzi na timu, itamkosti.

Hussein Mteremko, Handeni

AZAM imwache Dube aende anakotaka na sio kusema anauzwa 700 milioni, hapa Bongo hakuna nyota wa hela hiyo. Azam wamesahau walivyowawabeba Fei Toto, Djuma Shaban na Yanick Bangala?

Barnabas Soseleje, Masasi

MIMI naona Yanga ndio inayomfaa zaidi Dube.

Ramadhan Juma, Kondoa

AZAM waache mchezo mchafu wa kuwarubuni wachezaji, sasa ona dhambi imeanza kuwatafuna wenyewe. Wakiendelea hivi mwishowe watatuharibia ligi yetu kama TFF haitakuwa makini nao.

Majuto Said, Dodoma

NASHAURI Dube aende Simba kwani atakuwa na muda wa kucheza kutokana na kikosi kilivyo, lakini pia ataisaidia timu hiyo.

Mdau

MIMI ni Mwanajangwani kindakindaki, nauliza Dube karudi kwao Zimbabwe au bado yupo Bongo?

Mawazo Leshata, Gairo

KULINGANA na Dube ameamua kuondoka basi itabidi awalipe Azam na kama hana uwezo basi apitishe bakuli.

Mdau

JAMAA kama ameamua kuachana na Azam basi ajiunge na Msimbazi, kule ndio timu sahihi kwake.

Shahibu Ndwata, Arusha

PRINCE Dube aende Yanga tu, huenda akatimiza ndoto zake.

Hassan Juma, Dar es Salaam

SIMBA kuna tatizo la ushambuliaji, viongozi wambebe Dube atatusaidia kwani anajua kufunga sana.

Utenga Olivo, Makuka Iringa