Dodoma Jiji yavunja mkataba na Makata, Masoud anukia

TAARIFA rasmi kutoka kwenye klabu ya Dodoma Jiji, imethibitisha kumfungashia virago, aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbwana Makata kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo.
Ndani ya michezo mitano iliyopita, Makata alijikuta akiongoza Dodoma Jiji kuambulia pointi moja tu dhidi ya Geita Gold na kukumbana na vipigo vinne, ikiwemo vitatu mfululizo ambavyo ni kama vilikoleza kuota nyasi kwa kibarua chake makao makuu ya nchi.
Taarifa rasmi iliyotolewa leo, Jumatano imeeleza kuwa,"Hatua hizi zimechukuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ya timu katika mashindano mbalimbali ya msimu huu wa 2021/22."
Haikuishia hapo, taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Fourtatus Johnstone iliendelea kwa kusema,"Klabu inapenda kutoa shukrani za dhati kwa kocha Mbwana Makata kwa mchango wake mkubwa kwenye timu yetu kila la kheri katika maisha yake mapya."
Licha ya kutothibitishwa lakini zipo taarifa kuwa viongozi wa Dodoma Jiji wapo kwenye hatua za mwisho za kumpa kibarua hicho, Masoud Djuma ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Simba.
Katika mchakato wa kumpata mrithi wa Makata inaelezwa kuwa Mmarekani, Melis Medo ambaye alikuwa akiinoa Coastal Union ya Tanga naye alikuwa miongoni mwa makocha ambao walikuwa wakipigiwa hesabu.
Pamoja na kufungashiwa virago vyake, Makata anatajwa kuwa kwenye rada za Polisi Tanzania hivyo lolote linaweza kutokea.
TAKWIMU ZA MASOUD
Masoud alikuwa Msaidizi wa Joseph Omog, Simba katika mechi 10 tu, timu ikishinda mechi sita, sare tatu na kufungwa moja kwa penalti 4-3 na Green Warriors katika hatua za awali za Kombe la ASFC.
Baada ya kutolewa na Green Warriors katika Kombe la TFF, Omog akafukuzwa na Masoud akakaimu Ukocha Mkuu, timu ikicheza mechi saba, kushinda nne, sare moja na kufungwa mbili kabla ya ujio wa Kocha mpya Mkuu, Mfaransa Pierre Lechantre.
Na wakati wa Lechantre Simba ilicheza mechi 22 na kushinda 14, sare saba na kufungwa moja kabla ya Mfaransa huyo kuondolewa na Masoud tena kuwa Kaimu Kocha Mkuu akiiongoza timu katika mechi nane na kushinda tano, kufungwa mbili na sare moja.
Na wakati wa Aussems, pamoja na zile mechi tatu ambazo hakusafiri, SImba imecheza jumla ya mechi 13, ikishinda saba, sare tano na kufungwa moja.