Dodoma Jiji, KMC vita ya nafasi Bara

Muktasari:

  • Dodoma ambayo huu utakuwa mchezo wake wa 23, ikishinda itasogea kutoka nafasi ya 10 iliyopo sasa na pointi 25 hadi ya nane na kuzishusha Namungo na Singida Fountain Gate zenye pointi 26 kila mmoja ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

LIGI Kuu Bara inaendelea tena leo kwa mchezo mmoja kupigwa ambapo Dodoma Jiji itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kucheza na KMC.

Dodoma ambayo huu utakuwa mchezo wake wa 23, ikishinda itasogea kutoka nafasi ya 10 iliyopo sasa na pointi 25 hadi ya nane na kuzishusha Namungo na Singida Fountain Gate zenye pointi 26 kila mmoja ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa upande wa KMC ambayo huu utakuwa mchezo wake wa 24, endapo itashinda itafikisha pointi 35 hivyo kusogea nafasi moja juu kutoka ya tano iliyopo sasa hadi ya nne na kuishusha Coastal yenye 33 itakayocheza na Yanga Jumamosi hii ya Aprili 27.

Timu zote zinakutana huku zikiwa na ubora na udhaifu unaofanana ambapo KMC licha ya kufunga mabao 25, imeruhusu nyavu zake kutikishwa mara 32 sawa na Dodoma Jiji ambayo safu yake ya ushambuliaji imefunga 16 na kuruhusu kufungwa 22.

KMC inamtegemea mshambuliaji wake nyota, Waziri Junior ambaye hadi sasa amefunga mabao 11 nyuma ya vinara Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam aliyefunga 14 na Stephane Aziz KI wa Yanga anayeongoza kwa kupachika mabao 15 ya Ligi Kuu.

Kwa upande wa Dodoma Jiji inamtegemea mshambuliaji, Hassan Mwaterema ambaye ndiye anayeongoza kwa mabao ndani ya timu hiyo akifunga manne nyuma ya Emmanuel Martin mwenye matatu, Paul Peter na Yassin Mgaza waliofunga mawili kila mmoja wao.

Dodoma Jiji chini ya Francis Baraza inapenda kutumia mfumo wa kujilinda zaidi wakati huo huo ikishambulia kwa kuwatumia mawinga wake Emmanuel Martin na Idd Kipwagile huku KMC ikifunguka na kushambulia jambo linaloigharimu timu hiyo kuruhusu bao.


BATO IKO HAPA!

Katika mchezo huu sehemu mbili kuu ndizo zitakazokuwa na ushindani zaidi ambapo ya kwanza ni eneo la kiungo na mawinga wa timu zote.

Wenyeji Dodoma Jiji inawategemea zaidi Mtenje Albano na Gustapha Saimon kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao huku kwa upande wa KMC ikiwategema Awesu Awesu na Ibrahim Elias ambao wamekuwa na kiwango bora hadi sasa katika michezo ya ligi.

Bato nyingine itakuwa pembeni baina ya timu hizo ambapo Rahim Shomary mwenye uwezo wa kuzuia na kwenda mbele kutengeneza mashambulizi atakutana na moja ya mawinga bora wa Dodoma wakiwemo, Emmanuel Martin au Iddi Kipagwile ambao ni wasumbufu.

REKODI ZIKO HIVI!

Rekodi zinaonyesha timu hizi zimekutana katika jumla ya michezo saba ya Ligi Kuu Bara tangu zilipoanza kukutana msimu wa 2020/2021 ambapo Dodoma imekuwa mbabe zaidi kwani imeshinda mitano kati ya hiyo huku kwa upande wa KMC ikishinda miwili tu.

Katika michezo minne mfululizo iliyopita baina ya timu hizo katika Ligi Kuu Bara, Dodoma imeshinda yote huku mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, KMC ilichapwa mabao 2-1, Novemba 3, mwaka jana.

KAULI ZA MAKOCHA

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji Mkenya, Francis Baraza alisema anatarajia mchezo mgumu ingawa lengo lao kubwa ni kupata pointi tatu.

"Baada ya mchezo wetu na Simba kuahirishwa tuliendelea na mazoezi ya kujiweka fiti, tunashukuru hadi sasa hakuna nyota wetu yeyote aliye majeruhi, tunaiheshimu KMC kutokana na ubora wake ila tupo tayari kupambania pointi tatu," alisema.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin alisema jambo kubwa ambalo amekuwa akilifanyia kazi katika uwanja wa mazoezi kwa siku za karibuni ni kutengeneza mizani sawa ya timu hiyo kuanzia eneo la kujilinda hadi la ushambuliaji.