Dodoma, Fountain na rekodi ya vipigo vikubwa Bara

Muktasari:
- Mbali na timu hizo, zingine zilizopokea vipigo vikubwa msimu huu ni KMC, Pamba Jiji, Tanzania Prisons, KenGold, Mashujaa na JKT Tanzania.
KATIKA timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu, Dodoma Jiji, Fountain Gate na Kagera Sugar, zinaongoza kwa kupokea vipigo vikubwa hadi sasa zikiwa zimebaki raundi mbili kuhitimisha msimu wa ligi hiyo.
Mbali na timu hizo, zingine zilizopokea vipigo vikubwa msimu huu ni KMC, Pamba Jiji, Tanzania Prisons, KenGold, Mashujaa na JKT Tanzania.
Ipo hivi, Dodoma Jiji inayoshika nafasi ya saba kwenye msimamo ikikusanya pointi 34, katika mechi 28 ilizocheza imepoteza tatu kwa vipigo vikubwa huku ikiruhusu mabao mengi zaidi kupitia vichapo hivyo ambayo ni 15. Ilianza kwa kufungwa 4-0 na Yanga, kisha Simba 6-0 na Azam 5-0.
Fountain Gate inafuatia kwa kupoteza mechi tatu kwa vipigo vikubwa ikiruhusu mabao 13, ikifungwa na Yanga mara mbili 4-0 na 5-0, pia ikafungwa 4-0 na Simba.
Wakati timu hizo mbili zikiruhusu idadi hiyo kubwa ya mabao kwa vipigo vikubwa, Kagera Sugar ambayo pia imepokea vipigo vitatu vikubwa, angalau imetikisa nyavu za wapinzani wake.
Kagera Sugar iliyoshuka daraja, imepoteza mechi tatu kwa vipigo vikubwa ikiruhusu mabao 13 huku yenyewe ikifunga manne. Ilifungwa 5-2 na Simba, 4-2 dhidi ya Azam na 4-0 kwa Yanga.
KMC pia imepokea vipigo vikubwa viwili ikifungwa 4-0 na Azam, kisha ikachapwa 6-1 na Yanga, huku Pamba Jiji nayo ikifungwa 4-0 na Yanga na ikapokea kichapo cha mabao 5-1 mbele ya Simba.
Tanzania Prisons imefungwa 4-0 na Yanga, kisha kipigo kama hicho ikikipata kwa Azam.
KenGold ambayo nayo imeshuka daraja, imeshuhudiwa mechi moja pekee ikipokea kichapo kizito kutoka kwa Yanga cha mabao 6-1, wakati Mashujaa ikichapwa 5-0 na Yanga, huku Tabora United ikiipiga JKT Tanzania mabao 4-2.
Wakati hali ikiwa hivyo, upande mwingine Yanga ndiyo inayoongoza kwa kugawa dozi nzito kwa wapinzani ikifanya hivyo mara tisa ikizifunga Fountain Gate (4-0 na 5-0), KMC (6-1), Pamba Jiji (4-0), Kagera Sugar (4-0), Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0), KenGold (6-1) na Mashujaa (5-0).
Simba na Azam, zimetoa vipigo vikubwa mara nne kila moja. Simba imezifunga Fountain Gate (4-0), Pamba Jiji (5-1), Kagera Sugar (5-2) na Dodoma Jiji (6-0). Kwa upande wa Azam, imezifunga KMC (4-0), Kagera Sugar (4-2), Tanzania Prisons (4-0) na Dodoma Jiji (5-0).