Djuma alainishiwa kazi Jangwani

Monday October 11 2021
djumaa pic
By Clezencia Tryphone

MASHINE mbili za Yanga zimetua jana nchini zikirejea ndani ya muda kufuatia ruhusa maalumu waliyopewa, lakini beki wao akafichua makali ya ukuta wao msimu huu, akisema imemlainishia kazi Jangwani, huku akiwataja mastaa wenzake kadhaa.

Beki wa kulia kutoka DR Congo, Djuma Shaban ameliambia Mwanaspoti, hatua muhimu katika ukuta wao ni jinsi wanavyokabiliana na makosa ambayo wanayafanya katika kila mchezo, lakini akifichua namna kazi yake iliyorahisishwa tangu aungane na wenzak kikosini Jangwani.

Djuma alirejea sambamba na winga Jesus Moloko wote wametimkia kwao DR Congo kwa ruhusa fupi wakirejea ndani ya muda waliopewa na kocha wao Nesreddine Nabi na beki huyo alisema uzoefu wa mabeki na kipa wao Diarra Djigui umekuwa silaha muhimu ya kusahihisha makosa yao na kwamba ubora huo utawabeba katika safu yao ya ulinzi iliyopo chini ya Nahodha Bakar Mwamnyeto.

“Sio kwamba hatufanyi makosa yapo makosa, lakini jambo zuri ni jinsi tunavyokumbushana na kusahihisha makosa ndani ya uwanja kutokana na kila mmoja amekuwa na uzoefu mkubwa na hii imefanya tuwe na kazi rahisi katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa,” alisema Djuma aliyecheza mechi zote mbili za Ligi Kuu, Yanga kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold.

“Ukiangalia kuanzia kwenye safu ya kiungo mpaka mabeki pia ubora wa Diarra (Djigui) umekuwa unasaidia timu nafikiri tukiendelea hivi tutafanya vizuri,” aliongeza.

Djuma alisema pia kucheza kwake kwa ukaribu na Moloko, waliyetua wote Yanga msimu huu kumemfanya asiwe na kazi kubwa ya ‘kumwaga’ maji kwani winga huyo amekuwa akitimiza wajibu wake, wakati wakisaidiana kutengeneza mashambulizi ya timu. Moloko ndiye aliyefunga bao dhidi ya Geita.

Advertisement


WADAU WAFUNGUKA

Kuhusu kukumbushana kwa mabeki hao wa Yanga imemfanya beki wa zamani wa timu hiyo, Fred Mbuna kusema ni hatua bora kwa mabeki wa timu hiyo endapo watacheza kwa kukumbushana na kujisahihisha makosa yao ndani ya mchezo.

“Kitu ambacho kinahitajika ni hicho anachosema Djuma mchezaji hutakiwi kusubiri kocha akurekebishe,mnapofanya makosa kitu kizuri ni kujisahihisha wenyewe kwa wenyewe pia nimeona wamekuwa wakikumbushana kwa kuelewana,” alisema Mbuna. Kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Akida Makunda alitoa mtazamo wake akisema; “Yanga kutoruhusu bao katika mechi hizi mbili kunatokana na udhaifu wa timu pinzani, binafsi naona bado beki yake inatakiwa kujijenga zaidi ili icheze kwa utulivu.”

Katika hatua nyingine Kocha Nabi na vijana wake baada ya tizi la nguvu kambini Avic, leo watashuka uwanjani kujipima nguvu dhidi ya JKU ya Zanzibar.Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Yanga, mchezo huo utapigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, ili kocha Nabi aangalie walichokuwa wanakifanya mazoezini baada ya kumaliza mechi ya pili ya Ligi Kuu.

Advertisement