Dili la Maabad lapinduka jioooni!

Muktasari:
- Maabad mwenye mabao matano katika Ligi Kuu, amemaliza mkataba aliokuwa nao na Wagosi, jambo lililoifanya Tabora Utd kufanya mazungumzo na klabu inayommiliki ya KVZ ya Zanzibar, lakini wakati ikiwa imeshafanya malipo ya kumbeba straika huyo, ghafla fedha zilirudishwa ili aendelee kubaki Coastal.
LILE dili la mshambuliaji nyota wa Coastal Union, Maabad Maulid aliyepo kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) inayoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 kutaka kutua Tabora United, limepinduka baada ya Wagosi kumng’ang’ania na kumbakisha kikosi kibabe.
Maabad mwenye mabao matano katika Ligi Kuu, amemaliza mkataba aliokuwa nao na Wagosi, jambo lililoifanya Tabora Utd kufanya mazungumzo na klabu inayommiliki ya KVZ ya Zanzibar, lakini wakati ikiwa imeshafanya malipo ya kumbeba straika huyo, ghafla fedha zilirudishwa ili aendelee kubaki Coastal.
Inaelezwa kuwa, baada ya makubaliano ya pande mbili Tabora ilikamilisha malipo ya usajili, lakini kabla ya mchezaji huyo kujiunga na kikosi hicho pesa hizo zilirudishwa kwa Nyuki kutokana na Coastal kuingilia kati kutaka kubaki naye ili amalizie msimu huu.
Ofisa Habari wa KVZ, Hassan Haji ndiye aliyefichua kukwama kwa dili hilo kwa kuliambia Mwanaspoti kuwa, lilifeli kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wa klabu hiyo.
Haji alisema ni kweli walikubaliana na Tabora United baada ya Coastal kutoeleweka kipindi mkataba unamalizika, lakini mambo yaliwekwa sawa na sasa Maabad ataendelea kuitumikia Coastal kama kawaida.
“Maabad amerudi tena Coastal kwa sasa na Tabora tuliiomba radhi na kuirejeshea pesa ilizotupatia, kwani kilichotokea kilikuwa nje ya uwezo wetu na masuala mengine ni ya klabu na uongozi wake, ila yule ni mchezaji wetu na ataendelea kucheza alipokuwa,” alisema Haji.