Dida aiumbua Ndanda kweupee

DIDA

NDANDA juzi Jumatano ilikumbana na kipigo kibaya zaidi dhidi ya Yanga katika Ligi Kuu Bara, lakini kama hiyo haitoshi Kipa Deogratius Munishi ‘Dida’  ni kama alikuwa miongoni mwa watazamaji kwenye mchezo huo.

Ipo hivi. Katika pambano hilo ndani ya dakika 90 kipa huyo alicheza mipira 15 tu, kati ya hiyo mitano pekee ndio iliyokuwa hatari langoni mwake na kuidaka, 10 alipewa pasi na mabeki wake.

Yanga iliishindilia Ndanda mabao 4-0, huku ikishambulia lango la timu hiyo muda mrefu, hadi kumfanya Dida awe likizo na kama angekuwa na Gazeti la Mwanaspoti jirani angeweza hata kusoma bila ya hofu.

Kipa huyo wa Yanga alisubiri hadi dakika ya saba ndipo alipocheza mpira wake wa kwanza aliopasiwa kwa kichwa na Vincent Bossou. Mipira ya mashambulizi aliyocheza Dida ni ule wa dakika 12, alipopangua faulo ya Ndanda kisha kuuwahi na kudaka tena. Dakika ya 34, Dida alipangua tena mpira wa faulo wa Kiggi Makasi, dakika ya 35 alitoka langoni kuuwahi mpira uliokuwa ukiwaniwa na Salum Telela na Bossou. Dakika ya 57, tena aliwahi na kucheza hatari iliyoletwa na Helbert Lukindo na kucheza tena faulo dakika ya 68. Dida pia alicheza tena mipira mingine tisa aliyorudishwa na mabeki Juma Abdul (dk 14 na 54), Bossou (dk 45 na 48), Emmanuel Martin (dk 17), Haruna Niyonzima dk 50), Kelvin Yondani (dk ya 54, 72 na 85). Kipa Jeremiah Kasubi wa Ndanda akuwa na wakati mgumu kwa nyota wa Yanga akaruhusu mabao 4-0.