Diarra, Aziz Ki washusha presha Yanga

SAA chache tangu Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi kusema hajawaona kambini mastaa wa wawili wa timu hiyo waliokuwa timu za taifa, kipa Diarra Djigui na Stephane Aziz Ki, nyota hao wameibuka mazoezini jioni hii na kushusha presha kwa mashabiki na benchi la ufundi kwa ujumla.

Yanga leo imefanya mazoezi yao ya mwisho kwenye Uwanja wa Avic Town, Kigamboni kujiandaa na mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns utakaopigwa kesho Jumamosi kuanzia saa 3:00 usiku Kwa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Wawili hao walikuwa katika mechi za kirafiki za kimataifa kwa timu za taifa Aziz Ki akiwa na Burkina Faso na Diarra akiitumikia Mali na kauli ya Gamondi mapema leo aliweka bayana hajawaona mazoezini na kwamba huenda wachezaji kuanzia watatu hadi wanne wataukosa mchezo huo wa kesho.

Hata hivyo, presha ya mashabiki wa timu hiyo imeshushwa na wawili hayo baada ya kuonekana katika mazoezini kabla ya mchezo huo dhidi ya Mamelodi.

Wawili hao ni wachezaji wa kikosi cha kwanza chini ya Gamondi kwenye mechi nyingi wamekuwa wakipewa kipaumbele cha kuanza kikosi cha kwanza.

Yanga inavaana na Mamelodi ikiwa ni mara ya pili baada ya awali kukutana katika mechi mbili za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2001 na Wasauzi kushindwa kwa jumla ya mabao 6-5 ikipata ushindi nyumbani wa 3-2 kisha kulazimisha sare ya 3-3 hapa Tanzania na kuwang'oa wenyeji wao.

Timu hizo zitarudiana wikiendi ijayo mjini Pretoria, Afrika Kusini na mshindi wa jumla atasonga mbele kuingia nusu fainali na kucheza na mshindi wa mchezo kati ya Esperance ya Tunisia au Asecv Mimosas ya Ivory Coast.