Diarra apata watetezi

Wednesday September 15 2021
diarra pic
By Olipa Assa

KIPA wa Yanga, Diarra Djigui amekingiwa kifua na mastaa wa zamani waliowataka mashabiki, kutofautisha utani wa mitandao wa “kudaka hadi mishale” na ufundi wa uwanjani utakaowapa kicheko baadae.

Djigui ameruhusu mabao matatu katika mechi zake mbili za kwanza za kiushindani langoni ambazo pia Yanga wamepoteza tangu asajiliwe kwa mbwembwe akisindikizwa na tambo zilizotolewa na Mjumbe wa Kamati ya Usajili, Injinia Hersi Said, aliyetania kwamba kipa huyo wa timu ya taifa ya Mali “anadaka mpaka mishale.”

Yanga ilifungwa 2-1 dhidi ya Zanaco ya Zambia katika mchezo wa kirafiki wakati wa Wiki ya Mwananchi na akatunguliwa na Rivers United katika kichapo cha 1-0 cha mechi ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo linaloonekana limeanza kuwa shida kwa mashabiki.

Watalamu wa soka wamejitokeza na kuliweka sawa hilo kwa kutoa elimu kwa mashabiki kwamba wakitaka timu isambaratike wasiishi maisha ya mtandao kwa kufananisha na ufundi wa kocha na wachezaji.

Straika wa zamani wa timu hiyo, Idd Moshi alisema Diarra ni binadamu kama wachezaji wengine na suala kudaka mishale ni utani uliotumika kuelezea ubora wa kipa huyo ambao tayari ameonyesha ishara zake kwa kuokoa hatari nyingi licha ya kufungwa mabao hayo.

“Kwa akili ya kawaida nani anaweza akadaka mshale! Ukiachana na hilo ni kipa mzuri anayehitaji muda wa kuzoea ligi ndipo atakapoisaidia Yanga, hivyo sioni sababu ya kumlaumu, utani wa mashabiki wa timu hizi za watani zisiguse masuala ya kiufundi,” alisema.

Advertisement

Hoja yake iliungwa mkono na mchezaji wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala aliyesema mashabiki wa Yanga wasimfananishe Djigui na Aishi Manula wa Simba ambaye tayari ameshawajua mabeki wake, hivyo inakuwa rahisi kuwapanga.

“Manula anajua ubora na udhaifu wa mabeki wake, hivyo anaweza akawa anawakumbusha mara kwa mara, sasa huyu Diarra nani kamzoea, unaposema mazoezi linatafsiri neno mazoea je!! walipata muda gani wa kuzoeana, ukiachana na hilo ndio kwanza anajifunza hata majina yao, lugha na mazingira kwa ujumla,” alisema Kasabalala na aliongeza kuwa;

“Kwanza timu ina washambuliaji, viungo washambuliaji na wakabaji, mabeki sasa unapomlaumu kipa unakuwa humtendei haki, binafsi naona ni mzuri na ni muda wa mashabiki wa Yanga kuwa watulivu na kuliacha benchi la ufundi lifanye kazi,” alisema.

Naye beki wa zamani wa timu hiyo, Bakari Malima alisema ni mapema kuanza kumtupia maneno ya kuvunja moyo kipa, badala yake anapaswa kupewa muda wa kuzoeana na mabeki wake ili kuijenga Yanga imara zaidi.

“Vitu vya mtandao vibakie kwa mashabiki, timu inapaswa kuzungumziwa kiufundi kwani wapinzani wetu wanafanya ufundi na siyo maneno ya mtandaoni,” alisema.

Advertisement