Diao kaingia kwenye mfumo Azam FC

KOCHA mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo ameweka wazi kwamba anafurahishwa na mikimbio ya mshambuliaji wake Alassane Diao baada ya kufunga bao moja katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKU.

Azam juzi usiku ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar na kushinda kwa mabao 3-1 mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Dabo alisema kwenye mchezo huo kipindi cha kwanza mshambuliaji huyo mikimbio yake ilikuwa midogo, lakini kile cha pili aliongeza na ndio maana akafunga bao.

“Mikimbio yake Diao ilikuwa ni mizuri hasa kipindi cha pili alikuwa anacheza ndani ya boksi na tukapata bao la kuongoza kupitia yeye,” alisema kocha huyo.

Akizungumzia mchezo, Dabo alisema ni kipimo tosha kwao wakati huu ambao Ligi Kuu Bara imesimama kwani kuna baadhi ya vitu ameviona vitawasaidia kuboresha.

“Kipimo kizuri kwetu wakati huu ligi ikiwa imesimama. Nimeona mazuri na mabaya ambayo natakiwa kuyafanyia kazi kwenye kikosi,” alisema.

Diao alifunga bao hilo dakika ya 47 akitumia vizuri mpira uliotemwa na kipa wa JKU, Haji Chafu na yeye kufunga. Mabao mengine ya Azam yalifungwa na Gibril Syllah aliyeweka wavuni mabao mawili na katika Ligi Kuu mshambuliaji huyo ameifungia timu yake bao moja.