Diamond noma... Mastaa Marekani wampa saluti

Muktasari:

KWA mujibu wa Diamond na menejimenti yake, kama kila kitu kitakwenda kama sawa mwisho wa mwaka huu ataachia albamu yake ya nne na huenda ikaitwa ‘Swahili Nation’.

KWA mujibu wa Diamond na menejimenti yake, kama kila kitu kitakwenda kama sawa mwisho wa mwaka huu ataachia albamu yake ya nne na huenda ikaitwa ‘Swahili Nation’.

Kwa sasa staa huyo, mshiriki wa tuzo za BET 2021 yuko nchini Marekani na kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii amekuwa akidokeza mambo anayofanya huko maandishi matatu ikiwa ni pamoja na kuonyesha wasanii anaokutana nao, wakiwa studio wakifanya kazi pamoja.

Kupitia vidokezo hivyo, mpaka sasa imethibitika kuwa albamu ya Diamond itakuwa na kolabo na wasanii wa Marekani wasiopongua wanne huku vidokezo vikionyesha wazi kuwa miongoni mwao ni Busta Rhymes, Wiz Khalifa, Snoop Doggy, Swae Lee na Alicia Keys pamoja na mumewe, prodyuza Swizz Beatz.

Mwanaspoti inawamulika kwa ukaribu mastaa hao huku ikijaribu kukuonyesha wasifu wao na namna kila msanii atakavyosaidia kuipandisha bei albamu hiyo kama atapata nafasi ya kuingiza sauti.


BUSTA RHYMES

Staa huyu mtaalamu wa kurap haraka haraka bila kuvuta pumzi yupo kwenye listi ya wasanii wanaotarajiwa kuingiza sauti kwenye albamu hiyo na hii ni kwa mujibu wa video iliyosambazwa mtandaoni ikimuonyesha Busta, Diamond na meneja wake Babu Tale wakiwa studio. Katika video hiyo pia Busta alimbatiza Diamond jina la Michael Jackson wa Afrika.

Wasifu wa Busta unaweza kupandisha bei albamu hiyo kwa sababu staa huyo amechaguliwa kuwania tuzo za Grammy miaka tisa mfululizo, kati ya mwaka 1997 hadi 2012, hata hivyo hakuwahi kushinda.

Katika tuzo za BET amewania kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 na kukusanya jumla ya tuzo sita. Pia kibao chake cha Got You All In Check kilitikisa kwenye chati za Billboard mwaka 1996 kwa kushika namba nane kwenye orodha ya ngoma 100 kali ndani ya Marekani.

Kama kweli sauti ya Busta itasikika kwenye albamu ya Diamond basi itakuwa ni mara ya pili sauti hiyo kufika Bongo kwani mara ya kwanza aliileta mwenyewe alipokuja kutumbuiza tamasha la Fiesta 2009.


WIZ KHALIFA

Kama jukumu la Busta kwenye albamu hiyo litakuwa ni kuwavuta wakongwe, basi kazi ya Wiz Khalifa itakuwa ni kuwanasa vijana.

Wiz Khalifa au Cameron Jibril Thomaz kama inavyoonekana kwenye vitambulisho vyake aliachia albamu ya kwanza mwaka 2006. Kisha akaendelea kufanya vizuri na kutengeneza hits song kama vile Black and Yellow, See You Again na We Dem Boyz pamoja na kutikisa chati na tuzo mbalimbali. Wiz ameachaguliwa kuwania Grammy kwa miaka mitano mfululizo, mwaka 2012 hadi 2016, lakini hakuwahi kushinda huku akimiliki tuzo ya BET aliyoipata mwaka 2011.

Mbali na muziki, kibongobongo Wiz Khalifa anafahamika pia kupitia mzazi mwenzake, mrembo Amber Rosa ambaye mastaa kadhaa wa kike Bongo wanatumia jina na muonekano wa kufanana naye, kwa mfano Amber Lulu ambaye zamani alikuwa na staili ya nywele inayofanana na Amber, nywele ndogo ndogo zilizopigwa rangi nyeupe.


SWAE LEE

Wanaopenda muziki wa Marekani wa sasa watavutwa kwenye albamu hiyo na Swae Lee kwa sababu ndiye msanii ambaye yupo kwenye midomo ya vijana wengi ukimlinganisha na mkongwe Busta na mkali Wiz Khalifa.

Kupitia Instagram yake, Diamond alipost picha inayoonyesha yeye na Swae Lee wakizungumza kwa ‘video call’ na chini aliandika ‘Sipati picha siku dunia itakaposikia tulichokifanya kwenye album yangu.’

Kwa Afrika Mashariki, Swae Lee anafahamika zaidi kupitia wimbo wa Unforgettable aliomshirikisha rapa French Montana wa Marekani. Umaarufu wa ngoma hiyo unakuja kwa sababu video yake ilifanyikia nchini Uganda, huku madansa watoto maarufu kama Ghetto Kids wakitumbuiza humo ndani.

Wimbo huo ulifikia namba 3 kwenye chati za Billboard ngoma 100 kali ndani ya Marekani mwaka 2017. Pia kwa miaka mitatu, yaani 2017, 2019 na 2020 Swae Lee alichaguliwa kuwania tuzo za Grammy lakini hakushinda.


ALICIA KEYS

Diamond na familia ya Alicia Keys ni ndugu hivyo hakuna namna staa huyo wa Marekani na mume wake Swizz Beatz ambaye ni prodyuza wakashindwa kuweka mkono kwenye albamu ijayo ya Diamond.

Tangu wamefika Marekani, Diamond amekuwa akishea video zinazomuonyesha akiwa karibu zaidi na prodyuza Swizz Beatz kama vile jamaa ndiye mwenyeji wao.

Wasifu wa Alicia kwa upande wa tuzo na mafanikio ya namba ni mkubwa sana ukilinganisha na wote waliotajwa hapo juu; anamiliki zaidi ya tuzo 15 za Grammy, saba za BET na rekodi kibao katika chati za Billboard.


SNOOP DOGG

Safari ya Mondi ilikutana na mkali wa Hip Hop, Snoop Dogg na walionekana wakiwa studio ikiashiria mwendelezo mzuri wa kufanya makubwa kwenye albamu yake hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki zake.

Ni bahati kwa Mondi ambaye anaonyesha kukubaliwa sana na wasanii wa Marekani na baada ya kuikosa tuzo ya BET ni kama ameamua kuanza maandalizi ya mapema kuhakikisha mwaka ujao anaibeba baada ya safari hii kwenda kwa Burna Boy.

Kutokana na umaarufu wa Snoop, ni wazi albamu mpya ya Mondi itasambaa sana na kuzidi kumfungulia milango kimataifa.


LIST ITAENDELEA

Kwa hali ilivyo inaonyesha wazi bado Diamond hajamaliza orodha yake, ni suala la muda tu na hadi atakaporejea nchini ndio kitaeleweka na ni wazi kwa sasa mashabiki wanahamu kubwa ya kusikia nini kitakuwa kwenye albamu hiyo.