Prime
Depu ampasua kichwa Barker
SIMBA inasaka mshambuliaji mpya lakini kuna straika mmoja yupo Yanga anampasua kichwa kocha wa Wekundu hao wa Msimbazi, akitamani kupata mtu aina yake.
Straika anayetajwa Simba ni Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ ambaye ameitumikia Yanga kwa miezi sita tu lakini kocha wa Simba, Steve Barker amewaambia mabosi wake kwamba anataka mtu mwenye sifa kama za raia huyo wa Angola.
Bosi mmoja wa juu wa Simba ameliambia Mwanaspoti kuwa, katika msako wa straika wao mpya wanatamani kupata mshambuliaji mwenye sifa kama za Depu ambaye atakuwa na akili kubwa ya umaliziaji kuliko utafutaji.
Alisema katika msako huo, Barker anatamani kupata mshambuliaji mwenye nguvu na ubunifu kwenye eneo la mwisho akisema anatamani kupata mtu kama Depu.
“Unamuona yule Depu, tunatafuta mtu kama yule, yule ni mshambuliaji halisi kabisa, angalia mabao ambayo anayafunga unaona ubunifu wa umaliziaji wake,” alisema bosi huyo wa Simba.
“Pale Yanga Depu ni kama wanamkosea, hapati watu wa kumfanya acheze kwa kulikaribia lango, viungo wanacheza naye mbali sana ndio maana mnaona hafungi sana, yaani anatumika kama Dube (Prince) sasa tofauti ya Dube ni kwamba anaweza kujitafutia kwa kuzunguka kwa umbali mrefu.”
Aidha bosi huyo aliongeza kuwa, Yanga kama itamuacha Depu, mshambuliaji huyo atawahi haraka kupata timu kutokana na ubora wake.
“Yanga kama ikimuacha Depu leo, basi kesho atapata timu mpya haraka kutokana na washambuliaji wengi hawana sifa kama zake, ukiwa na mshambuliaji kama yule unatakiwa kutafuta viungo tu wabunifu wa kumpa mipira,” alisema bosi huyo.
Mshambuliaji huyo ambaye ameifungia Yanga mabao tisa kwenye Ligi Kuu Bara akicheza mechi 18, pia ana moja Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiwa na asisti mbili. Alitua kikosini hapo kipindi cha dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Radomiak ya Poland.
Kumekuwa na taarifa kwamba, Depu kuna uwezekano akapewa mkono wa kwaheri ndani ya Yanga ikielezwa kwamba ameshindwa kufikia matarajio ya klabu wakati anatua.
Wakati hayo yakijiri, Simba imekuwa ikisaka mshambuliaji kwa ajili ya kuelekea msimu ujao baada ya Jonathan Sowah kuwa kwenye mgogoro na klabu hiyo huku ikielezwa atasitishiwa mkataba wake.
Pia Seleman Mwalimu ambaye alibaki kama mshambuliaji wa mwisho kikosini hapo katika msimu uliomalizika akitupia mabao tisa kwenye ligi akicheza mechi 25, mkataba wake wa mkopo wa mwaka mmoja klabuni hapo umeisha, hivyo anarejea Wydad Casablanca ya Morocco na kama Simba itamuhitaji, inabidi mazungumzo mapya yafanyike.
Hata hivyo, ni kama Barker anaonekana kutoridhishwa na kiwango cha Mwalimu kwani katika kikosi chake hatua za mwisho za kumaliza msimu, alikuwa akimtumia kama mchezaji wa akiba, huku akianza na Elie Mpanzu eneo la mwisho la kushambulia ambaye kiasili yeye ni kiungo.