Dante atajwa Simba, Azam

Muktasari:
Chanzo kimoja kutoka kwa mtu wa karibu na Dante aliliambia Mwanaspoti, mchezaji huyo hivi sasa anajua kabisa kwamba maisha yake ndani ya Yanga ni mafupi kutokana na mabosi wa klabu hiyo kumchukulia poa.
UNAAMBIWA ukikiona cha nini wenzako wanajiuliza watakipata lini na hilo ndilo linaloendelea hivi sasa kwa beki wa Yanga, Andrew Vincent 'Dante', baada ya kutajwa kuwa ameanza kupigiwa hesabu na klabu za Azam na Simba.
Mwanaspoti limezipata ni kwamba nyota huyu ambaye anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu jina lake lipo mikononi mwa vigogo wa Simba na Azam fc kwaajili ya kuwa nae msimu ujao.
Inaelezwa Simba walikuwa wanataka kumsajili katika dirisha dogo na walikuwa wanafuatilia kila hatua ya kesi yake (madai ya pesa zake za usajili) na dili hilo liliyeyuka baada ya Dante kuelewana na Yanga jinsi ya kulipana lakini hivi sasa wameanza upya kuhitaji saini ya beki huyo baada ya kugundua kwamba mchezaji huyo amebakiza miezi miwili katika mkataba wake.
Simba wanataka kumsajili Dante kutokana na uzoefu wake alionao kuanzia katika timu ya Taifa mpaka ngazi ya klabu, lakini wakati huo huo mabosi wa Azam nao wanataka kumchukua mchezaji huyo ili kwenda kuongeza changamoto kwenye nafasi ya beki wa kati ambapo wamezoeleka kucheza Aggrey Morris na Yakub Mohamed.
Chanzo kimoja kutoka kwa mtu wa karibu na Dante aliliambia Mwanaspoti, mchezaji huyo hivi sasa anajua kabisa kwamba maisha yake ndani ya Yanga ni mafupi kutokana na mabosi wa klabu hiyo kumchukulia poa.
"Ni kweli kwamba Simba na Azam zimeonyesha nia ya kumuhitaji, kuna baadhi ya viongozi wanawatuma watu kutaka kufahamu hali ya afya yake, bado hawajukubaliana lolote mpaka hivi sasa," alisema.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba kitu kingine ambacho kinaweza kumfanya Dante ashindwe kuendelea na Yanga kutokana na mabosi wa Yanga kumchukulia poa.
"Unajua Dante hajamaliziwa pesa zake, ilikuwa amaliziwe mwezi wa tatu lakini haijwa hivyo, unazani kutakuwa na mkataba mpya huku nyuma ukiwa unawadai?," alihoji.
DANTE AFUNGUKA
Alipotafutwa Dante mwenyewe kuzungumzia tetesi hizo za yeye kuhitajika na Azam pamoja na Simba amesema, yeye ni mchezaji na anachoangalia ni maslahi yake.
"Bado nina mkataba mimi mpaka hivi sasa japo umebaki kidogo kumalizika, lakini mimi nategemea mpira kwahiyo ninachoangalia ni maslahi yangu," amesema.
Akizungumzia upande wa kuendelea kudai pesa zake kwa Yanga amesema; "Hilo siwezi kulizungumzia kwa muda huu."
Kwa upande wa Afisa Mtendaji mkuu wa Simba, Senzo Mbatha yeye alisema "Mpaka hivi sasa bado hatujaanza usajili rasmi katika kikosi chetu, sio mtu wa kuamini katika tetesi tusubili,".
Kama Dante atatua kwenye kikosi cha Simba basi kutokana na uzoefu wake wa mechi za kimataifa na kukabiliana na presha zote anaweza kutoa changamoto kwa mabeki wa sasa Pascal Wawa na Erasto Nyoni baada ya waliopo Kennedy Juma na Yusuph Mlipili kuonekana kushindwa huku ikiwa ni hivyo hivyo kwa Azam baada ya mabeki Oscar Masai na Abdallah Kheri 'Sebo' kushindwa kabisa kuonyesha cheche zao mbele ya Morris na Yakub.