Dalali atoa neno Simba, matawi mambo freshi

MWENYEKITI wa zamani wa klabu ya Simba, Hassan Dalali amewapongeza viongozi walioko madarakani kwa sasa kuhusu kuendeleza tamasha kubwa la Simba Day ambalo alilianzisha.

Dalali alianzisha Simba Day 2009 na lilifanyika kwa mara ya kwanza Agosti 8, mwaka huo na mpaka unasoma hapa litakuwa limetimiza miaka tisa tangu kuanzishwa kwake.

“Nilianzisha Simba Day kwa lengo la kupata pesa ya kulipia kile kiwanja pale Bunju na tunashukuru tulifanikisha hilo na tukapata hati miliki ya kiwanja kile, lengo lingine ilikuwa kuwatambulisha wachezaji wa Simba ambao miaka ya nyuma walikuwa wakitambulishwa katika mkutano mkuu,” anasema.

“Tulitaka pia mashabiki na wanachama kutoka katika mikoa mbalimbali au matawi tofauti ili waweze kufahamiana jambo ambalo kweli tulikuwa tukifanikiwa kila linapofanyika tamasha hili.

“Ninaomba viongozi wa sasa mbali na hayo ambayo tulikuwa tunafanya sisi wakati wetu wao wanatakiwa kutumia kama chanzo cha pesa kwa kuuza jezi na mambo mengine mengi ambayo wakianzisha kitakuwa kitega uchumi cha kukitegemea kabisa,” anasema Dalali.

Mwanaspoti mbali ya kuzungumza na Dalali lilitembea baadhi ya matawi makubwa hapa nchini ya Simba na kuzungumza na viongozi wao wakieleza hisia zao kuhusu wiki nzima ya Simba na mambo ambayo watafanya kwa Jamii.

UBUNGO TERMINAL

Mwenyekiti wa tawi la Ubungo Terminal, Ayubu Simba anasema kwa upande wao wamejipanga kuhakikisha wanafanya vitu vya tofauti katika wiki yote ambayo yatakuwa kama muendelezo katika miaka yote inayokuja.

Simba alisema kwanza matukio wanayohusika nayo ni shughuli za kijamii ambazo zilianza Agosti 4, walikwenda kufanya usafi katika Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani (Ubungo Bus Terminal) ambapo tawi hilo lilianzishwa.

Anasema kwa upande wao wanashukuru uongozi wa Simba kuwapatia heshima ya kuwachagua kama tawi bora la mwaka katika Tuzo za MO Simba Awards ambazo zilitolewa kwa wachezaji wa wadau wengine wa timu hiyo.

“Heshima kubwa ambayo tumepatia ya kupata tuzo na limetufanya kuongeza kasi yetu ya kuwepo na Simba kukote ambako itakwenda kucheza mechi na kutoa mchango wowote ambao upo ndani ya uwezo wetu,” anasema.

“Tawi letu tangu kuanzishwa linatimiza miaka 10 na tutafanya sherehe kwa kushirikiana na wachezaji, viongozi na wadau wote wa Simba na baada ya hapo tutakuwa tunafanya matokeo muhimu ya kuisaidia jamii ambayo yatakuwa ya mwendelezo kwetu,” alisema Simba.

MPIRA PESA

Tawi la Mpira Pesa linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Ostadhi Masoud katika wiki ya Simba, wamefanya matukio makubwa mawili ambayo yote yalihusisha shughuli za kijamii.

Masoud anasema kwa ukubwa wa tawi lao, Ijumaa iliyopita walikwenda katika kituo kimoja cha watoto yatima kilichopo Tabata Dar es Salaam na kuwapatia unga wa ngano kilogramu 25 viroba vitatu, mafuta ya kupikia kindoo kimoja na sukari kilogramu 15.

“Baada ya matokeo hayo siku ya Jumapili au Jumatatu tulikwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoa damu kwa kuwapatia wahitaji,” alisema Masoud na kuongeza tawi lao limekuwa na desturi ya kufanya shughuli za kijamii kila Simba Day.

SIMBA UKAWA

Katibu wa tawi la Simba Ukawa, Hasara Mbalike alisema kwa upande wao msimu huu hawakujaliwa kufanya mambo makubwa lakini wamejipanga kupeleka kikundi cha ushangiliaji kilicho kamili siku ya mechi.

Mbalike anasema wao walikutana kama kikundi na kufanya vikao vizito kuhakikisha msimu unaoanza wanakwenda mahala popote Simba itakapokuwa inacheza mechi ili kuwashangilia mwanzo mwisho bila kujali motokeo yoyote ya uwanjani.

“Hatuna tofauti na uongozi wala yoyote ambaye anahusika na Simba hatuna makubwa ya kufanya katika msimu huu ila Simba itakapokuwa na sisi tutakuwepo kuishangilia na kila tunapopata nafasi tutaongea na wachezaji wajitume ili kushinda mechi na kutupa raha ya kushangilia zaidi,” anasema Mbalike.