Daktari Mtibwa afunguka hali ya kipa Makaka

DAKTARI wa Mtibwa Sugar, Lawrance Mushi amesema hali ya kipa wa timu hiyo, Mohamed Makaka inaendelea vizuri kwa sasa ingawa bado anaendelea kufanyiwa vipimo zaidi vya kimatibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, General.

Nyota huyo alishindwa kuendelea na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji juzi Ijumaa uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dakika ya 25 tu baada ya kuanguka ghafla na nafasi yake kuchukuliwa na Razack Shekimweri.

Mushi alisema hali ya kipa huyo kwa sasa inazidi kuimarika vizuri ila anaendelea kufanyiwa vipimo ili kutambua nini sababu iliyomfanya kuanguka ghafla na kushindwa kuendelea na mchezo huo.

“Alianguka ghafla bila ya mpira wowote wa kugombania na mchezaji na baada ya kumuangalia ili kumpatia huduma ya kwanza uwanjani nikagundua alipoteza fahamu, hivyo tukamuwahisha hospitali na anaendelea vizuri.”

Mushi aliongeza jambo hilo ni la kawaida kutokea kwa wachezaji, hivyo baada ya kumfanyia vipimo zaidi watatoa majibu juu ya kilichotokea ila kwa sasa wapenzi na mashabiki wa soka watambue hali yake imeimarika.

Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Habibu Kondo alisema wanamuombea apone haraka ili aendelee na majukumu yake kwani licha ya makipa wengi waliokuwa nao ila yeye ndio muhimili na vijana hujifunza kutokea kwake.