Dakika 450 za mtafutano kwa makocha 11 Ligi Kuu

Baadhi ya wachezaji wa Mtibwa Sugar iliyopo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara wakifanya mazoezi

Muktasari:

  • Hadi sasa Yanga anayetetea taji lake kwa msimu wa tatu mfululizo, ndiye kinara kwa pointi 65, Azam akifuatia kwa alama 57, Simba akiwa nafasi ya tatu kwa pointi 53 na Coastal Union akifunga ‘Top Four’ kwa pointi 34.

WAKATI zikisalia mechi tano kumaliza Ligi Kuu msimu wa 2023/24, presha ipo kwa timu 11 ambazo zinapaswa kuchanga vyema karata zake ili kubaki salama.

Hadi sasa Yanga anayetetea taji lake kwa msimu wa tatu mfululizo, ndiye kinara kwa pointi 65, Azam akifuatia kwa alama 57, Simba akiwa nafasi ya tatu kwa pointi 53 na Coastal Union akifunga ‘Top Four’ kwa pointi 34.

Timu za Simba na Dodoma Jiji ndizo zimecheza mechi pungufu (24) huku nyingine zilizobaki zikishuka uwanjani mara 25 na kubakiwa na michezo mitano pekee kuamua hatma yao.

Pamoja na Mtibwa Sugar kuwa mkiani kwa alama 17 na kupewa nafasi kubwa ya kushuka daraja msimu huu, lakini lolote linaweza kutokea iwapo itajipapatua kushinsa michezo iliyobaki.

Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya tano inaweza kufikiwa na vibonde waliopo nafasi nne za chini iwapo watashinda michezo yao iliyobaki, wakati huohuo wakiwaombea mabaya waliopo juu yao.

Timu za Geita Gold (24), Mashujaa na Tabora United zenye pointi 23 iwapo zitashinda michezo iliyobaki zinaweza kuzishusha Coastal Union (34) na KMC wenye alama 33.

Mtibwa Sugar walio mkiani watakutana na Tabora United, Yanga na Namungo (nyumbani) kisha kumaliza na Mashujaa na Ihefu ugenini, huku ikihitaji kulipa kisasi kwa wapinzani wanne.

Katika mechi za raundi ya kwanza, Mtibwa ilipoteza mbele ya Ihefu 3-2, ikafa 1-0 kwa Namungo, ikalala 4-1 dhidi ya Yanga na 2-1 kwa Tabora United, huku ikishinda 1-0 dhidi ya Mashujaa.

Kwa upande wa Tabora United ambao ni msimu wao wa kwanza Ligi Kuu, watakuwa na Mtibwa Sugar, Yanga na Namungo (ugenini) kisha Mashujaa na Ihefu nyumbani.

Wapinzani hao katika mechi za kwanza, walipoteza mechi mbili dhidi ya Yanga 3-0 na Ihefu 2-1, ikashinda moja dhidi ya Mtibwa 2-1 na sare mbili dhidi ya Namungo 1-1 na Mashujaa 1-1.

Mashujaa nao ambao ni msimu wa kwanza Ligi Kuu, watakuwa na mechi tatu nyumbani dhidi ya KMC, Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji na mbili ugenini kwa Tabora United na Tanzania Prisons.

Geita Gold walio nafasi ya 13, watakuwa na kibarua kizito dhidi ya vigogo Namungo, Simba na Singida FG (ugenini) na Azam, Coastal Union na Namungo nyumbani kuweza kutoboa.

Dodoma Jiji walio nafasi ya 10 kwa pointi 28 watakuwa na kibarua dhidi ya Prisons, Namungo, Simba itakaokutana nao mechi mbili, Yanga na Mashujaa kisha kusubiri hatma yao.

KMC nao watakuwa na kazi nzito ugenini kwa mechi tatu dhidi ya Mashujaa, Simba na Coastal Union na mbili nyumbani mbele ya Azam na Singida FG kisha kusikilizia matokeo ya walio chini yao.

Prisons nao watakuwa na mechi tatu ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, Namungo na Yanga, huku ikicheza nyumbani miwili kwa Ihefu na Mashujaa ikihitaji japo pointi sita kuwa salama.

Coastal Union walio moto kwa sasa, watakuwa na mechi tatu nyumbani dhidi ya Singida FG, JKT Tanzania na KMC na kutoka miwili mbele ya Geita Gold na Kagera Sugar.

Akizungumzia presha iliyopo mbele yao, Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdalah Mohamed ‘Baresi’ amesema pamoja na matokeo waliyonayo kutokuwa mazuri, lakini bado haijaisha hadi iishe na kwamba mechi zilizobaki kitaeleweka.

“Tunajua presha ilivyo, lakini hatujakata tamaa kwakuwa nafasi tunayo ya kupambania kubaki salama, kimsingi ni kuwaandaa wachezaji kiakili ili wanapokuwa mchezoni kazi iwe moja,” amesema Baresi.

Kocha Mkuu wa Ihefu, (Singida Black Stars), Mecky Maxime amesema licha ya kutoanza vizuri msimu, lakini kwa sasa wanaona mabadiliko mazuri na kwamba ishu ya kushuka daraja haipo.

“Tupo kwenye hesabu kali kuhakikisha michezo iliyobaki tunavuna pointi 15 ambazo zitatuweka salama kwa ajili ya msimu ujao, hiyo presha inatupa changamoto kupambana,” amesema Maxime.