Dakika 270 zaibua matumaini Kagera

Muktasari:
- Kagera katika mechi hizo tatu zilizopita ambazo sawa na dakika 270 ikiwa chini ya Medo, imekusanya pointi nne kutokana na kushinda 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, sare ya 1-1 dhidi ya Pamba Jiji na kufungwa 1-0 dhidi ya Coastal Union.
OFISA Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabit Kandoro amesema anaridhishwa na mwenendo wa timu hiyo katika matokeo ya mechi tatu zilizopita akimtaja kocha mpya, Melis Medo kuwa ndiye chanzo.
Kagera katika mechi hizo tatu zilizopita ambazo sawa na dakika 270 ikiwa chini ya Medo, imekusanya pointi nne kutokana na kushinda 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, sare ya 1-1 dhidi ya Pamba Jiji na kufungwa 1-0 dhidi ya Coastal Union.
Timu hiyo imecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara ikishika nafasi ya 14 katika msimamo, imeshinda mbili na sare mbili huku ikipoteza michezo sita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kandoro alisema, anaridhishwa na mwanzo mzuri wa kocha huyo kwani amefanikiwa kuiunganisha timu hiyo.
“Tunaona mwanga mkubwa na tunakubaliana naye kwamba timu yetu inahitaji maboresho makubwa kwenye dirisha dogo, lakini safari ya mapambano haitakoma mpaka tufikie wakati huo.
“Maandalizi yetu yanaridhisha kwamba tutakapokutana na Azam kuna kitu tofauti timu yetu itakionyesha Novemba 23 ambapo tutakuwa ugenini,” alisema Kandoro.
Kikosi hicho ambacho awali kilikuwa chini ya Paul Nkata, kocha huyo hadi anaondoka alikuwa amekiongoza katika mechi saba, kikishinda mchezo mmoja, sare moja na kupoteza tano.
Mchezo ujao Kagera itacheza na Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, huku ikiwa na rekodi ya kipigo cha mabao 5-1 msimu uliopita katika dimba hilo hilo.