Dabo: No Dube, No Diao, No Problem!

Muktasari:

  • Dabo amesema sababu kubwa ya timu hiyo kupata matokeo chanya katika michezo yao ya hivi karibuni ya mashindano yote bila ya mshambuliaji asilia ni kutokana na kutengeneza balansi kwenye aina ya uchezaji wa kikosi hicho kitu kilicholipa.

AZAM imecheza mechi 11 bila ya mshambuliaji asilia, kutokana na Allasane Diao kuwa majeruhi, huku Prince Dube akiisusa timu akilazimisha kuondoka, lakini hilo halijaizuia timu hiyo kupata matokeo mazuri na kocha Youssouph Dabo amefichua kilichombeba licha ya kutokuwa na nyota hao tegemeo.

Dabo amesema sababu kubwa ya timu hiyo kupata matokeo chanya katika michezo yao ya hivi karibuni ya mashindano yote bila ya mshambuliaji asilia ni kutokana na kutengeneza balansi kwenye aina ya uchezaji wa kikosi hicho kitu kilicholipa.

Mara ya mwisho kwa timu hiyo kucheza na mshambuliaji ilikuwa Februari 9, mwaka huu wakati kikosi hicho kikilazimishwa sare ya 1-1 na Simba, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza huku bao lao likifungwa na Prince Dube.

Mchezo huo ndio ambao ulikuwa wa mwisho kwa Prince Dube kucheza ndani ya timu hiyo baada ya kutokuwa na maelewano mazuri na viongozi wanaoshinikiza mkataba wake unaisha 2026 huku yeye akisisitiza mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.

Azam iliyopo nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 54, imecheza jumla ya michezo 11 ya mashindano yote bila ya mshambuliaji asilia ambapo kati yake imeshinda saba na kutoka sare minne ikifunga mabao 17 na kuruhusu matano.

Akizungumzia hilo, Dabo alisema baada ya washambuliaji wengi kuumia huku wakiwa na michezo muhimu ilibidi kutoa nafasi kwa kila mmoja wao.

“Ni pengo kucheza kwa muda mrefu bila ya mshambuliaji asilia ila nashukuru wachezaji wote wamekuwa wakijitoa kupigania timu, ilikuwa haina jinsi kwa sababu ni katikati ya msimu hivyo tunapambana na hali tuliyokuwa nayo kwa sasa,” alisema.

Nyota mwingine mbali na Dube aliyekuwa na mabao saba ya Ligi Kuu Bara hadi sasa aliyeumia ni Msenegali, Alassane Diao ambaye alifanyiwa upasuaji wa goti kufuatia kupata majeraha ya anterior cruciate ligament (ACL), Machi 15, mwaka huu.

Licha ya kuumia kwao, nyota kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekuwa muhimili mkubwa akihusika katika mabao 20 ya Ligi Kuu Bara baada ya kufunga 14 na kuchangia asisti sita huku Kipre Junior akifunga manane na kutoa asisti nane.