Dabi yampa Oumba mbinu za ushindi fainali FA

Muktasari:
- Ouma ameliambia Mwanaspoti alikuwa na dakika 90 za kuisoma Yanga ikiifunga Simba kwa mabao 2-0 huku akibaini ubora na upungufu wa Yanga na kuahidi kuwa mbinu bora ndio zitakazoipa Singida Black Stars taji la kwanza msimu huu.
DAKIKA 90 za mchezo kati ya wenyeji Yanga dhidi ya watani zao Simba zimemtosha kocha wa Singida Black Stars, David Ouma kutambua ni wapi anatakiwa kufanyia kazi kabla ya kuvaana na timu hiyo Jumapili hii na kushinda.
Ouma ameliambia Mwanaspoti alikuwa na dakika 90 za kuisoma Yanga ikiifunga Simba kwa mabao 2-0 huku akibaini ubora na upungufu wa Yanga na kuahidi kuwa mbinu bora ndio zitakazoipa Singida Black Stars taji la kwanza msimu huu.
Jumapili hii Yanga itacheza dhidi ya Singida Black Stars katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
“Huwezi kukutana na timu bora ambayo imethibitisha hilo kwa kutwaa ubingwa bila ya kuunda mbinu za kuisoma, nimefanya hivyo kwa kuitazama ikikutana na wapinzani wao Simba nafikiri nimegundua wapi ni bora na wapi wana mapungufu, bado nina muda zaidi kabla ya kuvaana nayo Jumapili,” alisema na kuongeza.
“Kila kitu kinaenda vizuri, tumetoka Singida tayari kwa kuiwahi Yanga Zanzibar, wachezaji wanatambua ubora wa Yanga na umuhimu wa mchezo huo kwa kulihitaji kombe, maandalizi sahihi na mbinu bora ndizo zitakazoamua mchezo huo.”
Ouma alisema haitakuwa fainali rahisi lakini anaamini wana nafasi ya kufanya vizuri na kutwaa taji lao la kwanza msimu huu kutokana na ubora wa mchezaji mmoja mmoja ndani ya kikosi chao.
“Yanga ni timu bora na ina wachezaji wengi wa kuamua matokeo lakini hata sisi sio wanyonge ukizingatia wachezaji wangu wana uchu wa kufikia mafanikio ya kutwaa taji baada ya kupata nafasi ya kucheza fainali utakuwa mchezo bora na wa ushindani,” alisema.
Singida inakabiliwa na rekodi ngumu ya kuivunja, kwani michuano hiyo iliporejea tena msimu wa 2015-2016, baada ya kutofanyika kwa kipindi cha miaka 13, tangu mwaka 2002, Yanga ndiyo imechukua mara nyingi zaidi ambazo ni nne huku msimu huu ikiingia fainali ikiwa bingwa mtetezi.
Timu nyingine zilizochukua ubingwa huo tangu kipindi hicho mbali na Yanga ni Simba, Mtibwa Sugar na Azam, jambo linalosubiriwa ni kuona kama Singida Black Stars itaandika rekodi mpya au itashindwa kutamba.
Tangu michuano hiyo iliporejea msimu wa 2015-2016, Yanga ndiyo timu inayoongoza kwa kuchukua ubingwa huo mara nyingi zaidi, baada ya kufanya hivyo mara nne, ikifuatiwa na wapinzani wao wakubwa Simba, waliolichukua taji hilo mara tatu.
Singida ilianza michuano hiyo hatua ya 64, bora kwa kuifunga Magnet FC zamani Malimao ya Dar es Salaam mabao 2-0, kisha 32, bora ikakutana na Mabingwa wa Mkoa wa Kagera, Leo Tena FC na kuichapa mabao 4-0 na kufuzu kibabe katika hatua ya 16, bora.
Hatua ya 16 bora, Singida ikakutana na KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara na kuichapa bao 1-0, huku hatua ya robo fainali ikaichapa Kagera Sugar mabao 2-0 na kufuzu nusu fainali, kisha kuiondosha Simba kwa kuifunga 3-1 na kufuzu hadi fainali.
Moja ya jambo la kipekee kwa Singida, tangu michuano hiyo imeanza msimu huu, imeruhusu bao moja tu ambalo ni la kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua, huku kwa upande wa wapinzani wao Yanga ikiwa hadi sasa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
Mbali na hilo, ila Singida inakabiliwa na mtihani wa kuvunja rekodi ya Yanga ya kutopoteza mechi ya Kombe la Shirikisho (FA), kwani kikosi hicho tangu mara ya mwisho kilipochapwa na Simba bao 1-0, Julai 25, 2021, hadi leo hakijapoteza.