Dabi ya Wakata Miwa, Makocha watambiana

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime na Nahodha wa timu hiyo, David Luhende wakizungumzia maandalizi ya timu yao kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

DABI ya Wakata Miwa, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itapigwa kesho katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 8 mchana huku makocha wa timu hizo wakitambiana kila mmoja akizitaka pointi tatu ili kikosi chake kiendelee kukwea juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa timu hizo kukutana msimu huu ambapo katika msimu uliopita Kagera Sugar ilishinda bao 1-0 Kaitaba na kupata sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Manungu.

Timu hizo zimecheza michezo 13 ya Ligi kuu msimu huu ambapo Mtibwa Sugar imevuna pointi 21 ikikamata nafasi ya sita wakati Kagera Sugar ikipata pointi 15 kwenye nafasi ya tisa.

Timu hizo zinaingia kwenye mtanange huo kesho zikiwa na rekodi nzuri ya matokeo kwenye michezo miwili iliyopita ambapo Kagera Sugar imevuna pointi nne ugenini dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons huku Mtibwa Sugar ikivuna alama sita baada ya kuzichapa Coastal Union na Polisi Tanzania.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi kuelekea mchezo huo ambao utakuwa ni wa tano tangu achukue mikoba ya Francis Baraza, Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ametamba kuwa wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo iliyopita na wamejiandaa kubakiza pointi tayu nyumbani.

Kipa wa Mtibwa Sugar, Razack Shekimweli (kushoto) na kocha msaidizi wa timu hiyo, Awadh Juma (katikati) wakielezea maandalizi ya kikosi chao kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Kagera Sugar.

Amesema anakwenda kukabiliana na timu ambayo ina benchi zuri la ufundi lenye makocha wanaomfahamu vyema aina yake ya ufundishaji wakiongozwa na Salum Mayanga hivyo utakuwa mchezo mgumu lakini amefanya maandalizi ya kutosha na vijana wake.

"Mchezo utakuwa mgumu wenzetu (Mtibwa Sugar) wana mwendelezo mzuri wa matokeo nacheza na mwalimu wangu Mayanga (Salum) ananifahamu na mimi namfahamu. Kikubwa tumejipanga kupata matokeo ili tusogee katika nafasi nzuri," amesema Maxime.

Naye Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma amesema wanakutana na timu ngumu inayocheza soka la kumiliki mchezo kwa asilimia kubwa dhidi ya wapinzani hivyo watakuwa na kazi ya ziada ya kufanya kuwazuia.

Amesema licha ya upinzani mkubwa uliopo wanahitaji ushindi katika mchezo huo ili waendelee kukamata nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu ambapo katika kufanikisha hilo wamewajenga kisaikolojia na kimbinu wachezaji wao waweze kufanikisha lengo hilo.

"Tunajua tunakwenda kucheza na timu inayomiliki mpira na tunajua soka la Maxime (Mecky) kwahiyo tunaingia kwa kumheshimu kwa kujua ni mwalimu na timu ya namna gani. Tumefanya mazoezi yetu vizuri tunaendelea kuwajenga kimorali na kimbinu wachezaji wetu ili tuendelee kukusanya pointi zitakazotuweka sehemu salama," amesema Juma.

Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo amesema maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri huku akiwaomba mashabiki wa soka jijini hapa kujitokeza kwa wingi kwani kiingilio ni Sh 3,000 tu.