CRDB yatia mabilioni Kombe la Shirikisho

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakionyesha hati za makubaliano ya udhamini wa Kombe la Shirikisho, baada ya kutia saini jijini Dar es Salaam, leo. 

Muktasari:

  • Benki hiyo itatoa Sh800 milioni kwa msimu wa 2024/2025,  Sh1 bilioni msimu wa 2025/2026 na kumalizia Sh1.2 bilioni msimu wa 2026/2027. 

MASHINDANO ya Kombe la Shirikisho Tanzania sasa yatajulikana kama CRDB Federation Cup baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu na benki ya CRDB kwa ajili ya kuwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo wenye thamani ya Sh3.76 bilioni.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Rais wa TFF, Wallace Karia amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni jambo litakalosaidia maendeleo ya mashindano hayo (zamani yakijulikana kama Kombe la Shirikisho la Azam) na soka kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Benki wa CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa tatu kutoka kulia) na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia (wa pili kushoto) wakiwa wameshika mfano wa hundi ya udhamini wa mashindano ya Kombe la Shirikisho.

"Azma ya TFF ni kuendeleza mashindano yetu mbalimbali. Haya ni mashindano ambayo yanashirikisha timu nyingi zaidi Tanzania. Kwa hiyo CRDB Bank Federation Cup ina zaidi ya timu 100 na mashindano haya yanaanzia katika ngazi ya wilaya," amesema Karia.

"Lakini pia zaidi ya nusu ya mechi za CRDB Bank Federation Cup zinaonyeshwa katika luninga. Niwahakikishie CRDB na wadhamini wetu wengine wote kuwa tumejipanga kuendeleza mpira wa miguu. Udhamini wa benki ya CRDB unakwenda kuongeza thamani ya Kombe la Shirikisho hivyo naamini klabu zitayapa uzito kwa vile bingwa wake anakwenda kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika."

Mkurugenzi mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuwa benki yake imefanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za TFF kuinua soka.

Nsekela amesema kuwa CRDB itatoa Dola 100,000 za Marekani(takriban Sh255 milioni) kwa TFF kwa lengo la kufanikisha mechi zilizobaki za msimu huu ambapo kwa sasa zipo timu 16.

Amesema benki hiyo pia itatoa Sh800 milioni kwa msimu wa 2024/2025 na baadaye Sh1 bilioni kwa msimu wa 2025/2026 na kumalizia Sh1.2 bilioni msimu wa 2026/2027. 

“Fedha hizi tutakazozitoa zinajumuisha zawadi ya mshindi wa michuano yaani timu bingwa, mchezaji bora wa kila mechi na mchezaji bora wa mzunguko, goli bora la mechi na goli bora la msimu pamoja na timu bora ya msimu,” amesema Nsekela. 

Fainali kupigwa Babati
Katika hatua nyingine TFF imetangaza kuwa fainali ya mashindano hayo mwaka huu itafanyikia Babati katika Uwanja wa Tanzanite.

Karia amesema uamuzi huo umechukuliwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo baada ya kuona kuwa uwanja huo unakidhi vigezo vya kuandaa mchezo huo.

"Tunapeleka mashindano haya kutoa shukrani na sapoti kwa juhudi ambazo zinafanywa na maeneo husika na kuendeleza mpira huko. Kuna baadhi ya mikoa warekebishe miundombinu ili tuweze kuwapa nafasi hiyo," amesema Karia.

Karia amesema kuwa kabla ya hatua hiyo ya fainali kutakuwa na mechi za hatua ya nusu fainali ambazo mojawapo itachezwa Mwanza.

"Uwanja ambao utachezwa nusu fainali nyingine bado hatujatangaza. Kuna mikoa ambayo tumeipa changamoto ya kuboresha miundombinu na utakaokidhi vigezo tutaupa fursa hiyo," amesema.

Ikumbukwe kwamba katika msimu uliopita fainali ya mashindano hayo ilichezwa katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambapo Yanga iliibuka bingwa baada ya kuifunga Azam FC kwa bao 1-0.