Covid-19 ilivyoishika pabaya Bandari FC

Muktasari:

Shughuli zote za kimichezo nchini zilisimama ikiwa ni jitihada za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona na kuwafanya wanamichezo kusalia majumbani.

BANDARI FC inafikiria kuwa ndiyo klabu iliyoathirika zaidi kati ya zile za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) wakati corona ilipotangazwa kuwa janga na kuwekwa kafyu.

Kwa nini Bandari ndiyo inayodai kuathirika zaidi ya nyengine? Kwenye mahojiano na Kocha Mkuu Ken Odhiambo alitoa sababu kadhaa za timu yake kuathirika kutokana na janga la corona na nini matarajio yake ruhusa ikitolewa ya kuruhusiwa kurudi uwanjani.

Siku ambayo tangazo la kafyu lilipotolewa, timu hiyo ya Bandari ilikuwa imepangiwa kucheza na Sofapaka kwenye mechi ya robo fainali ya Ngao ya FKF katika shindano ambalo mshindi wake ndiye anayewakilisha nchi kwenye dimba la Caf Confederation Cup.

Mechi hiyo haikufanyika kama ilivyotarajiwa na hivyo, Bandari ambayo bingwa wa dimba hilo ikakosa fursa ya kupigania kuhifadhi taji lao waliloshinda msimu wa 2018-2019 na ikashuiriki kwenye mashindano hayo ya barani Afrika.

“Tulijipanga vilivyo kuhakikisha tunahifadhi taji letu na tuweze kujiandikishia tena tikiti ya kushiriki kwenye mashi ndano ya Kombe la Caf, lakini kutokana na ugonjwa huo wa Covid-19, mashindano hayo hayakuendelea,” akasema Odhiambo.

Mkufunzi huyo wa klabu ya pekee ya jimbo la Pwani inayoshiriki kwenye ligi ya KPL amesema kuwa wakati wa kutangazwsa kwa kafyu, wachezaji wake walikuwa kwenye fomu ya hali ya juu ambapo ilikuwa tayari imeshinda mechi tatu na kutoka sare mchezo mmoja wa ligi.

“Hakika vijana wangu walikuwa wamekuwa kwenye fomu nzuri ambayo nina hakika tungemaliza kwenye nafasi mojawapo tatu za juu na pia tulikuwa na tamaa ya kubeba tena Ngao ya FKF,” akasema.

Jambo ambalo liliwapa moyo mkubwa mashabiki wa timu hiyo kuwa timu yao itaweza kufanya vizuri ni kuwa tangu Odhiambo ashikilie hatamu ya kurudi kuifunza tena, haikuwahi kufungwa mechi yoyote kati ya tano ilizocheza.

Bandari iliweza kupata ushindi kwenye mechi nne, tatu za ligi, kuichapa KCB kwa mabao 2-1 katika mechi mbili, moja ya nyumbani na nyengine ya ugenini, ikailaza Kariobangi Sharks 1-0 na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Homeboys. Iliichapa Ogopa FC 2-0 mechi ya Ngao ya FKF.

Kwa wakati huu, Odhiambo anasema kwa kipindi hicho cha corona, wachezaji wameathirika kwa sababu kadhaa zikiwemo za kutokuwa pamoja kama familia, kukosa safari ambapo wanakuwako pamoja kwenye mabasi na kukosa marupurupu wanapocheza mechi.

“Kwa muda huu, wachezaji wanapata mishahara yao pekee lakini hawapati marupurupu ambayo huwasaidia wao na jamii zao. Pia wanasoka wangu wanakosa ile raha ya kushangiliwa na mashabiki wao haswa wanapocheza mechi za nyumbani,” akasema.

Mbali na hayo, wanaathirika kwa njia moja ama nyingine kuwa na wasiwasi wa kutembeleana kama ilivyo desturi zao na kufanya mazoezi ya pamoja amabayo yanawasaidia kuinua vipaji vya uchezaji wao.

“Ni jambo la uhakika kuwa japo wanafanya mazoezi, lakini kubwa wanachofaidika nacho zaidi ni zoezi la physical lakini wanakosa mazoezi ya kiakili (mental), kiufundi (technical), na mbinu (tactical),” akasema Odhiambo.

Hata hivyo, Odhiambo anasema ana imani kubwa kwa kuwa wachezaji wake wote isipokuwa, Fred Nkata wako mjini Mombasa na mara itakapotangazwa ruhusa ya wachezaji kuingia uwanjani, atakauwa hana shida na wanaweza kurudia hali zao kwa haraka. Kwa wakati huu, kocha Odhiambo anawapitia wanasoka wake kuangalia jinsi wanavyofanya mazoezi kama alivyowapangia.