Congo United yaongoza kwa usajili

Timu ya Tinga Tinga ya Kanda ya Nairobi Kati ikiwa na kutoka kushoto Denson Mburu, James Gitau, George Were, Antony Kimani (mwamuzi) na Joseph Nene wakishangilia ushindi wa timu yao katika mashindano ya 'Guinness Football Challenge'. Timu hiyo ni miongoni mwa zaidi ya timu 1,500 zinazoshiriki mashindano hayo kote nchini. PICHA NA ABDULRAHMAN SHERIFF
ABDULRAHMAN SHERIFF CONGO United ya Mombasa ndiyo klabu inayoongoza kwa kutema na kusajili wanasoka wengi nchini Kenya. Kulingana na takwimu zilizotolewa na wasimamizi wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Congo United imewatema wanasoka 10 na imesajili wanasoka saba wakati wapinzani wao, Bandari imewaacha wanasoka wanne na kusajili wapya idadi kama hiyo. Congo United imewatema Ronald Okoth, Phillipe Ouma, Alex Nyamweno, Mohammed Hussein, Abdalla Hussein, Kaakan June, Mohamed Zakivy, Andrew Onangwe na Nathan Munai. Mkurugenzi wa Ufundi wa Congo United, Aref Baghazally aliiambia Mwanaspoti mapema wiki hii kwamba walikubaliana kumuuza mshambuliaji wao Wycliffe Ochomo kwa klabu ya Gor Mahia kwa gharama ya Sh. 200,000, lakini KPL ilikuwa bado haijaidhinisha usajili huo. Nayo Tusker FC imewatema Anthony Khadudu, Oscar Kadenge, Athman Bori, Robert Syongoh, Joseph Njuguna na Alex Ikaanga wakati Bandari imewatema George King, Saidi Madidima, Michael Mataza na Eric Oduor. AFC Leopards imewatoa kikosini Selenge Mangili, Douglas Okumu, Israel Ogude, Itubu Imbem na Evans Wandera wakati Sony Sugar imemwacha mchezaji wake wa kiungo, Daniel Odhiambo. Kulingana na KPL, imeidhinisha usajili wa wachezaji saba wa Congo – Mohammed Bazenga kutoka Admiral, Mohamed Mwachidoni (Kilifi Stars), Frank Nwojo (Nigeria), Farid Mohammed Admiral), Salim Khamis (Admiral), Kevin “Keegan” Ngugi (Chemelil Sugar) na Ben Barasa (Bungoma United). Wachezaji wanne wa Bandari walioidhinishwa na KPL ni mlinzi Eric Ochieng, kipa Wycliffe Kasuya (waliotolewa na Red Berets) na viungo Ali Ahmed Breik na Evans Wandera kutoka AFC Leopards. Kiungo wa Gor Mahia, Ibrahim Kitawi alisajiliwa na Tusker FC.