Clatous chota Chama afichua siri Jangwani

Muktasari:

  • Klabu ya Yanga inaanza usaili wa wagombea wake leo Alhamisi kwenye klabu ikiwa ni maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ambao unatarajiwa kufanyika Januari 13 mwakani.

ASIKUAMBIE mtu kwa sasa jina linalotajwa midomoni mwa mashabiki wa soka ni kiungo Clatous Chama, Mzambia huyo amewapa kiburi Wekundu wa Msimbazi na kuwafanya mabosi wake kutamba kwa kufanikiwa kumsajili msimu huu.

Hata hivyo, licha ya Simba kushangilia mautundu ya kiungo huyo fundi, mwenyewe amefichua alivyonusurika kutua Yanga mapema kabla ya kutua Msimbazi.

Chama anakiri ilibaki kidogo tu atue Jangwani kama sio mabosi wa Msimbazi kumwahi mapema.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chama alisema wakati Yanga ikiwa na Kocha George Lwandamina alibakiza hatua chache kukubali dili la kujiunga na timu hiyo.

Chama alisema alifanya kazi na Lwandamina wakiwa Zesco na kocha huyo alipoondoka na kujiunga na Yanga aliamini naye atakuwa njiani kumfuata nyuma.

Chama alisema baada ya Lwandamina kutua Yanga alimgusia angetaka kumsajili lakini baada ya kufika Yanga mambo yakawa kimya. Alisema baada ya muda akapata dili jingine la kujiunga na timu moja ya Misri ambapo alimuaga Lwandamina kuwa hataweza kuungana naye tena.

“Hapa Tanzania niliwahi kuja na Zesco kwa mwaliko wa Simba na tukacheza kwenye lile Tamasha la Simba Day,” alisema Chama.

“Kuna wakati niliona nimekaribia kuja kufanya kazi hapa lakini niliamini ningekuja kucheza Yanga wakati kocha wao akiwa Lwandamina.

“Wakati anaondoka kule Zesco anakuja huku Yanga aliniambia atanichukua na mimi nilishakaa tayari kusubiri kumfuata.

“Alipofika huku sikujua kipi kiliendelea, alikuwa akinisisitiza ananihitaji bahati mbaya wakati nasubiri nikapata ofa nyingine ya kwenda Misri. Lwandamina kwangu ni baba ni zaidi ya kocha ni kama alivyo huyu Aussems (Patrick) wanajua kuishi na mchezaji kama mtoto wake.

Chama anayeichezea Timu ya Taifa ya Zambia ameifungia Simba mabao matano, matatu katika mechi za kimataifa na mawili ya Ligi Kuu Bara, huku akiwa gumzo kwa mashabiki.