City yaizamisha Azam Sokoine ikitinga nne bora

Muktasari:

  • Ushindi huo umeitoa City nafasi ya saba hadi kutinga 'Top Four' kwa pointi 31 huku Azam wakibaki nafasi yao ya tatu kwa alama 32.

Mbeya. Baada ya kukwama katika mchezo wake uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar 1-0, leo Jumanne Mbeya City imefanya kweli kwa kuwazamisha Azam FC 2-1 na kupanda nafasi nne za juu.

Ushindi huo unaifanya Mbeya City kuwatambia wapinzani hao msimu huu kwa kuchukua pointi nne baada ya mechi ya raundi ya kwanza iliyopigwa Chamazi Dar es Salaam kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa, ulianza kwa kupooza, huku kila timu  ikionekana kumsoma mpinzani lakini baadaye Azam walimiliki mpira na kufanya mashambulizi kadhaa lakini mabeki wakiongozwa na Hamad Waziri walikuwa makini kuharibu mipango.

Mbeya City walicharuka na kuanza kujibu mashambulizi lakini kazi nzuri ya Makipa na  mabeki waliweza kudhibiti hatari zote na dakika 45 za kwanza kumalizika kwa nguvu sawa ya bila kufungana.

Kipindi cha pili wenyeji City walirejea uwanjani na mzuka mwingi huku wakipeleka mashambulizi kwa wapinzani na dakika ya 51, Juma Shemvuni aliipatia bao la kuongoza baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Azam na mfungaji huyo kuukwamisha mpira wavuni.

Bao hilo lilionekana kuwachanganya Azam ambao walianza kupoteza mipira kadhaa na kuwafanya City kuongeza nguvu na dakika ya 81 Eliud Ambokile kunyoosha shuti lililomshinda Kipa wa Azam, Ahmed Suleiman na kuamsha shangwe kwa mashabiki wake.

Hata hivyo Azam walitulia kwa dakika za mwisho na kuwapelekea moto Mbeya City na dakika ya 88, Ayoub Lyanga aliyetokea benchi aliipatia bao Azam kwa shuti kutokea winga ya kushoto na kumuacha Kipa, Lameck Kanyonga ameshika kichwa.

Kwa matokeo hayo, City wanachumpa hadi nafasi ya nne kwa pointi 31 sawa na Geita Gold wakiwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga huku Azam wakibaki nafasi yao ya tatu kwa alama 32.