Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chipukizi hawa tishio Ligi Kuu Bara

Muktasari:

Ushindani huo wa timu za Ligi Kuu hapana shaka utaenda sambamba na ule wa wachezaji ambao kila mmoja atakuwa akipambana ili kutangaza jina lake na kujitengenezea mazingira ya kupata malisho mazuri siku za usoni.

Dar es Salaam. Pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2019/2020 limefunguliwa rasmi mwishoni mwa wiki hii ambapo timu 20 zitawania taji ambalo kwa sasa linashikwa na Simba.
Ushindani huo wa timu za Ligi Kuu hapana shaka utaenda sambamba na ule wa wachezaji ambao kila mmoja atakuwa akipambana ili kutangaza jina lake na kujitengenezea mazingira ya kupata malisho mazuri siku za usoni.
Wapo wachezaji ambao wanatazamwa zaidi kuwa wanaweza kutamba na kuzibeba timu zao kutokana na ubora na kiwango walichoonyesha siku za nyuma ingawa pia wapo wale ambao huenda wakachemsha.
Spoti Mikiki leo inakuangazia wachezaji saba wenye umri mdogo ambao huenda wakaitumia vyema Ligi Kuu msimu huu, kuyapa chati majina yao katika ramani ya soka.

Rashid Juma (Simba)
Ana umri wa miaka 19 hivi sasa na alianza rasmi kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, baada ya kupandiswa katika kikosi cha wakubwa akitokea timu ya vijana ya Simba ‘Simba B’.
Anaweza kucheza vyema kama winga na amekuwa akimkosha Kocha Patrick Aussems ambaye baadhi ya nyakati alikuwa akijaribu kumtumia kama beki wa pembeni.
Hata hivyo, ana kibarua kigumu cha kupata nafasi mbele ya mawinga Deo Kanda, Miraji Athumani na Cletous Chama lakini kama akipata nafasi ya kucheza, msimu huu unaweza kumpa chati.

Oscar Masai (Azam)
Ni mchezaji anayecheza kwa nidhamu na bidii ya hali ya juu licha ya umri mdogo  na ukosefu wa kutosha, hana hofu ya kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani.
Baada ya kucheza kwa mkopo kwenye timu kadhaa, safari hii amepandishwa kwenye kikosi cha wakubwa cha Azam FC na kupata nafasi moja kwa moja kutokana na majeraha ya nyota wawili wanaocheza kwenye nafasi ha beki wa kati, Aggrey Morris na David Mwantika.
Akiendelea kupata nafasi atazidi kuimarika zaidi na anaweza kuwa mmoja wa mabeki tegemeo watakaotamba.

Hashimu Manyanya (Namungo)
Winga msumbufu wa Namungo ambaye alitoa mchango mkubwa kwenye kikosi cha timu hiyo msimu uliopita ambao walifanikiwa kumaliza wakiwa vinara wa Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza jambo liliowapa tiketi ya kushiriki Ligi Kuu msimu huu.
Silaha kubwa inayoweza kumbeba Manyanya ni kasi yake, chenga, pasi na krosi zenye macho na pia uwezo wa kufumania nyavu pindi anapokaribia lango la timu pinzani.
Ana umri wa miaka 23 na msimu uliopita kwenye Ligi Daraja la Kwanza alipachika mabao manane (8) huku akipiga pasi 14 zilizozaa mabao.

Riphat Msuya  (Mtibwa)
Ni kijana aliye na umri wa miaka 20 mwenye uwezo wa hali ya juu wa kufumania nyavu kila anapopata nafasi ndani ya eneo la hatari la timu pinzani.
Msimu uliopita hakupata sana nafasi ya kucheza kutokana na majeraha lakini pia ushindani wa namba uliokuwepo kwenye kikosi cha Mtibwa kutokana na uwepo wa nyota kama Kelvin Sabato, Japhary Kibaya, Stamil Mbonde na Juma Liuzio.
Kuondoka kwa Sabato ‘Kiduku’ aliyetimkia Gwambina FC kunaweza kuwa neema kwake ikiwa atajituma na kufanya vizuri ndani ya uwanja.

Luka Kikoti (Namungo)
Wilayani Ruangwa, mashabiki wa soka wale wa Namungo FC wanamuita kwa jina la utani ‘Mtakatifu Luka Kikoti’ kutokana na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu za timu pinzani
Ikiwa atamudu kuhamisha ubora alioonyesha kwenye Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu, ni wazi kwamba mabeki wa timu pinzani watapata wakati mgumu kukabiliana naye.

Paul Godfrey ‘Boxer’   (Yanga)
Alipandishwa katika kikosi cha kwanza cha Yanga msimu uliopita akitokea timu ya vijana, lakini alionyesha kiwango bora kilichomkosha kila mmoja.
Ameendelea kuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza cha Yanga na ana nafasi kubwa ya kuwa na namba ya kudumu upande wa beki ya kulia.
Kama hatokumbana na majeruhi, Boxer mwenye umri wa miaka 19, ni mchezaji ambaye ataisaidia vilivyo Yanga lakini pia atajiweka katika mazingira mazuri ya kupata nafasi ya kuteuliwa kwenye timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.

Ismail Mhesa (Mtibwa)
Ana umri wa miaka 22 na ni zao la kikosi cha vijana cha Mtibwa Sugar ambayo ilimpika hadi akapata nafasi ya kucheza kwenye mechi za mashindano zinazohusu timu ya wakubwa
Anafanya vizuri katika nafasi ya winga ambayo ndio amekuwa akiicheza kwa muda mrefu kutokana na kasi, chenga na kupiga krosi na uwezo wake wa kumiliki mpira.
Amekuwa lulu ya kocha Zubery Katwila ambaye amekuwa akimpanga mara kwa mara na kama ataitumia vyema fursa hiyo ni wazi kwamba msimu jina lake litatikisa msimu huu.

Bakari Mwamnyeto (Coastal Union)
Ni beki anayecheza timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 na katika Ligi Kuu yupo kikosi cha Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Mwamnyeto ana uwezo wa hali ya juu wa kukabiliana na kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani na huenda nyota yake ikazidi kung’aa msimu huu.