Chikola, Yanga kuna kitu kinaendelea

Muktasari:
- Inadaiwa tayari nyota huyo mwenye mabao saba na asisti mbili katika Ligi Kuu Bara, amesaini mkataba wa awali na Yanga iliyokuwa inamfukuzia tangu msimu huu ulipoanza.
INGAWA ni siri, lakini taarifa zilizoifikia Mwanaspoti ni kwamba mshambuliaji wa Tabora United, Offen Chikola na Yanga kuna kitu kinaendelea ikiwa ni mipango ya kujiandaa kwa msimu ujao.
Inadaiwa tayari nyota huyo mwenye mabao saba na asisti mbili katika Ligi Kuu Bara, amesaini mkataba wa awali na Yanga iliyokuwa inamfukuzia tangu msimu huu ulipoanza.
Chanzo cha ndani kutoka Yanga kinasema mchezaji huyo keshasaini mkataba wa awali huku uongozi ukisubiri kukamilisha baadhi ya mambo ili kumalizana naye.
Endapo dili lake litakamilika katika nafasi yake Yanga alikuwapo Stephane Aziz Ki anayeondoka na msimu uliopita alikuwa MVP aliyemaliza na mabao 21 huku msimu huu akifunga tisa na asisti saba, lakini pia kuna Pacome Zouzoua aliyefunga tisa na asisti tisa, Clatous Chama aliyefunga manne na Shekhan Khamis ambaye hajacheza mechi nyingi.
Kwa upande wa Chikola amehusika na mabao tisa msimu huu, huku timu anayoichezea ikishika nafasi ya tano, na imefanya Yanga kumtazama kama mzawa anayeweza kuongeza nguvu katika kikosi.
“Tumefanya naye mazungumzo yamefikia pazuri na ameshasaini mkataba wa awali. Kila kitu kikikaa sawa basi anaweza akawa sehemu ya kikosi chetu kwa msimu ujao,” kilisema chanzo cha kuaminika.
Hata hivyo, Chikola ambaye amekuwa akipigiwa hesabu na timu kadhaa ikiwamo Simba, Azam na JKT Tanzania mwenyewe hakuwa tayari kuzungumza chochote, lakini rafiki yake wa karibuni alisema kuna mazungumzo yaliyoanza baina ya nyota hiyo na klabu kadhaa bila kuziweka hadharani.