Chikola azichambua dakika 540 ngumu Tabora

Muktasari:
- Timu hiyo inayoshika nafasi tano kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 37, mara ya mwisho kuapata ushindi ilikuwa ni ilipoilaza Dodoma Jiji 1-0 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, shukrani kwa bao la kujifunga la Dissan Galiwango wa Dodoma Jiji katika dakika ya 35.
FEBRUARI 28, 2025, ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa Tabora United kupata ushindi katika Ligi Kuu Bara, baada ya hapo imecheza mechi sita mfululizo sawa na dakika 540 ikiambulia vichapo huku kiungo wa kikosi hicho, Offen Chikola akitoa neno.
Timu hiyo inayoshika nafasi tano kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 37, mara ya mwisho kuapata ushindi ilikuwa ni ilipoilaza Dodoma Jiji 1-0 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, shukrani kwa bao la kujifunga la Dissan Galiwango wa Dodoma Jiji katika dakika ya 35.
Baada ya hapo timu hiyo imepoteza mechi sita mfululizo ikifunga bao moja tu kupitia Offen Chikola, huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13. Matokeo ya mechi hizo ni; Tabora United 1-2 JKT Tanzania, Tabora United 0-3 Yanga, Pamba Jiji 1-0 Tabora United, Mashujaa 3-0 Tabora United, Singida Black Stars 3-0 Tabora United na Tabora United 0-1 KMC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chikola alisema matokeo wanayoyapata ni kipindi cha mpito, wao kama wachezaji wanapambana lakini ubora wa wapinzani unawaadhibu.
“Hatufurahishwi na matokeo tunayoyapata, tumekuwa tukipambana kuhakikisha tunakuwa bora lakini tunazidiwa na timu pinzani, tumekaa na benchi la ufundi na kukubaliana kwa kupeana mbinu sahihi, tunaamini mechi mbili za mwisho za ligi tutarudi tukiwa imara,” alisema na kuongeza:
“Tumeshindwa kufikia malengo kwa sababu ya matokeo ambayo sio rafiki kwetu, lakini hilo halituondoi kwenye kupambania timu kuwa bora, kwenye mechi mbili zilizobaki tunatarajia ugumu lakini hatutakubali kugawa pointi.”
Tabora United ipo nafasi ya tano kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 28 ikikusanya pointi 37, imebakiza mechi mbili dhidi ya Azam FC na Coastal Union ambazo zote itacheza ugenini.
Moja ya sapraizi kubwa ambazo Nyuki hao wa Tabora wamefanya msimu huu, ni kuifunga Yanga mabao 3-1, kati ya mechi 10 ambazo wameshinda hadi sasa.