Championship sasa kuna hesabu za vidole

Muktasari:
- Pamoja na ushindani huo, lakini timu zilizoshuka daraja msimu uliopita, Mtibwa Sugar na Geita Gold zimeonekana kuwa na moto zikiwa nafasi mbili za juu kwa pointi 19 kwa 17.
UKIPIGWA tu unaachwa. Ndivyo unaweza kusema kuelezea mtifuano ulivyo kwenye Championship baada ya kushuhudia mechi nane zilizochezwa, huku timu sita zikikimbizana kwa jasho kileleni.
Pamoja na ushindani huo, lakini timu zilizoshuka daraja msimu uliopita, Mtibwa Sugar na Geita Gold zimeonekana kuwa na moto zikiwa nafasi mbili za juu kwa pointi 19 kwa 17.
Timu za TMA, Songea United (zamani FGA Talent), Mbeya City na Stand United zimeonekana kukamiana kwa kila mmoja akivuna pointi 15 zikitofautiana wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Pia Mbeya Kwanza, Bigman (zamani Mwadui) hazipo nyuma zikiwa zimevuna alama 14, huku Mbuni FC wakiwa na pointi 12 nafasi ya tisa na Green Warriors akifunga ‘Top Ten’ kwa pointi 10.
Licha ya upinzani huo, timu za Transit Camp, Kiluvya na African Sports zimeweka rekodi ya kucheza dakika 720 bila kuonja ushindi ikiwa ni sare na vichapo na kuwa nafasi tatu za mwisho.
Kocha Mkuu wa TMA, Maka Mwalwisi alisema licha ya ushindani huo, lakini bado matarajio yao msimu huu ni kupanda Ligi Kuu baada ya kukosa nafasi hiyo msimu uliopita.
“Msimu uliopita tulikubali kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kwetu kushiriki tukaishia nafasi ya nne, msimu huu hatutaki kukosea popote badala yake kucheza Ligi Kuu,” alisema Mwalwisi.
Kwa upande wa kocha wa Geita Gold, Aman Josiah alisema ushindani huo unafanya kila mmoja kujipanga kushinda mechi zake, akieleza kuwa ni mapema sana kuelezea ishu ya kupanda Ligi Kuu.
“Kila timu malengo yake ni kupanda daraja, lakini kwetu ni mapema tukikamilisha mechi zaidi ya 20, tunaweza kuona muelekeo rasmi tuendapo, vijana wako fiti,” alisema Josiah.