Chama, Baleke wabadili gia Simba

Muktasari:

  • Wachezaji wa Simba wamepewa mapumziko ya siku tano baada ya kukamilisha kazi ngumu ya kuivusha timu hiyo robo fainali Ligi ya mabingwa Afrika msimu huu huku nyota wengine wakiwa kwenye majukumu ya timu za taifa.

BAADA ya kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mastaa wa Simba wamekula kiapo kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi hatua inayofuata ili kuendelea kuweka rekodi nzuri kwenye mashindano hayo huku wakikiri kuwa wanamlima mrefu wa kuupanda.

Wachezaji wa Simba wamepewa mapumziko ya siku tano baada ya kukamilisha kazi ngumu ya kuivusha timu hiyo robo fainali Ligi ya mabingwa Afrika msimu huu huku nyota wengine wakiwa kwenye majukumu ya timu za taifa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema wamekamilisha lengo la kwanza sasa wanasahau matokeo hayo na kuwekeza nguvu zaidi hatua inayofuata.

Kiungo fundi wa Simba mwenye mabao manne na pasi moja ya bao kwenye Ligi ya mabingwa Afrika, Clatous Chama alisema kutokana na malengo yao ilikuwa lazima timu hiyo ifike robo fainali ya michuano hiyo.

Chama alisema anajisikia vizuri kufunga mabao matatu kwenye mechi iliyoivusha Simba hatua ya makundi na kuweka rekodi nzuri kwa timu pamoja na upande wake.

Alisema kufunga kwenye michezo mikubwa kama hiyo ya CAF, ni kutokana na mchango na ushirikiano kwa wachezaji wenzake hadi hilo linakamilika na timu kupata inachohitaji.

“Tunahitaji kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano haya ila sasa hilo limekwisha akili na nguvu tunazielekeza kwenye hatua nyingine, ila naomba niwapongeze wapenzi na mashabiki wa Simba kwa mchango wao mkubwa,” alisema Chama aliyeitwa kwenye timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’.

Jean Baleke alisema kuna kazi kubwa anahitaji kufanya zaidi ndani ya Simba kufunga mabao mawili kwenye mechi na Horoya ni sehemu ya kile alichokuwa anatamani kukufanya ndani ya Simba.

“Kufunga mabao matano kwenye michezo miwili mfululizo ya kikosi cha Simba si kitu rahisi ila binafsi naamini naweza kuongeza nguvu na kufanya hivi mara kwa mara, sasa tunabadilisha gia tunawaza zaidi hatua ya robo fainali,” alisema Baleke mwenye mabao mawili Ligi ya Mabingwa Afrika na kuongeza;
“Hadi hatua hii niwashukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wetu kwani kila mmoja kwa nafasi yake amefanya hivi hadi kufikia mafanikio haya.”

Wakati huo huo, Sadio Kanoute alisema jambo kubwa kwake si kufunga mabao mawili bali kuona timu inafikia yale mafanikio iliyokuwa imejipangia kabla ya msimu kuanza.

“Hatukuanza vizuri kwenye mashindano haya ya CAF, ila tunashukuru Mungu tumemaliza kwa furaha na timu kufika robo fainali sasa nguvu zetu ni kwenda hatua ya mbele zaidi na kuweka rekodi nyingine,” alisema Sadio.