Chama atia neno uteuzi Stars

Muktasari:

  • NYOTA wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Rashid Idd 'Chama'  ameungana na baadhi ya wadau na mashabiki walioshangazwa kutoitwa kwa mabeki Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwenye kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda.

MWANZA. NYOTA wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Rashid Idd 'Chama'  ameungana na baadhi ya wadau na mashabiki walioshangazwa kutoitwa kwa mabeki Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwenye kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda.

Kocha wa Stars, Adel Amrouche raia wa Algeria mapema wiki hii alitaja kikosi cha wachezaji 31 kitakachoivaa Uganda, Machi 24 mjini Kampala na kurudiana Machi 28 jijini Dar es Salaam huku nafasi za mabeki hao wa Simba zikichukuliwa na Yahya Mbegu (Ihefu) na Datius Peter wa Kagera Sugar.

Chama aliyekuwa miongoni mwa wachezaji wa Stars iliyocheza AFCON ya mwaka 1980 nchini Nigeria, alisema nyota walioitwa, lakini alitarajia kuwaona baadhi ya wachezaji walio kwenye kiwango kizuri, huku akiwashauri wote waliopata hiyo nafasi kutambua wamebeba bendera ya taifa na wapambane kwani taifa linawategea.

“Mimi naona kama wachezaji waliochaguliwa siyo wabaya lakini kuna wachezaji wameachwa sijui tatizo ni nini maana nashindwa kusema kwa sababu sijui wameachwa kwa tatizo gani mfano Sure boy (Abubakar Salum), Shabalala (Mohamed Hussein) na Shomari Kapombe walistaili kuwepo,” alisema Chama.

Kocha wa zamani wa Toto Africans na Mbao, John Tegete, aliungana na Chama na kudai uteuzi huo una kasoro ndogo kufuatia baadhi ya wachezaji wenye uzoefu na michuano ya kimataifa kuachwa huku akimpa mtihani kocha huyo mpya kujifunza kupitia mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda.

“Timu ya taifa siyo mbaya isipokuwa uteuzi kidogo una kasoro tunakwenda kwenye mashindano iweje wachaguliwe wachezaji wasio na uzoefu wakaachwa wazoefu ambao wameonyesha uwezo mkubwa kwenye mashindano yote wanayocheza,”

“Hiyo ni njia ya kuwakatisha tamaa wachezaji ambao tena wanajituma sana kwenye michezo yote wanayocheza. Ni vizuri kama hao wachezaji wangechaguliwa kwenye michezo ya kirafiki na siyo ya kimashindano,” alisema Tegete.