CAF yailima Yanga faini Sh82 milioni
Muktasari:
- Mechi hiyo ilichezwa kwenye Aprili 30 kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam ambapo Rivers walitoa malalamiko yao siku moja kabla ya mechi hiyo baada ya kumaliza mazoezi yao uwanjani hapo.
KLABU ya Yanga imetozwa faini ya jumla ya Dola 35,000 na Caf ambayo ni zaidi ya Sh 82 milioni kwa makosa mbalimbali yanayodaiwa kufanywa katika mechi yao ya robo fainali kati yao na Rivers United ya Nigeria.
Mechi hiyo ilichezwa Aprili 30, 2023 kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam ambapo Rivers walitoa malalamiko yao siku moja kabla ya mechi hiyo baada ya kumaliza mazoezi yao uwanjani hapo.
Rivers United walilalamika gari yao kuvunjwa vioo na kuibiwa dola 5000 huku wakidai pia kupuliziwa dawa.
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), iliyokutana Mei 4 mwaka huu, imeipiga faini Yanga kwa madai ya kuhusika kuwasha vitochi na kupiga mafataki uwanjani ambapo faini yake ni dola 10,000.
Faini nyingine ni Dola 25,000 kwa madai ya kupuliza dawa kwenye gari la timu ambalo walilitumia Rivers United walipokuwa mazoezini. Caf imeilekeza Yanga kulipa fedha hizo ndani ya siku 60 tangu kutolewa kwa adhabu hiyo.
Aidha Caf imetoa nafasi kwa Yanga kukata rufaa ndani ya siku tatu tangu kutolewa kwa adhabu hiyo na wakishindwa kukata rufaa ndani ya muda elekezi basi watatakiwa kulipa faini hiyo kama walivyoelekezwa.