Cadena aanza kuona mwanga Simba

Muktasari:

  • Simba ilikuwa imecheza jumla ya mechi 28 tangu Aprili 27 mwaka jana bila kupoteza mechi za Ligi Kuu Bara kabla ya kufumuliwa na Yanga mabao 5-1, ikiwa imetumia siku 373.

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Daniel Cadena amesema kwa namna wachezaji wa timu hiyo walivyocheza dhidi ya Namungo jana imempa picha namana wanavyoyafanyia kazi wanayowaelekeza mazoezini na anaamini wataendelea kuwa bora zaidi na kuwatuliza mashabiki akiwataka wawe na imani nao.

Cadena, aliyeajiriwa Simba kama kocha wa makipa amepewa dhamana ya kuinoa timu hiyo baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Roberto Oliveira 'Robertinho' kusitishiwa mkataba na kurejea kwao Brazili usiku wa kuamkia leo Ijumaa.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo raia wa Hispania, amesema ataendelea kuwatumia wachezaji wote waliosajiliwa ndani ya kikosi hicho ili wawe bora katika mchezo muda wote.

Katika mchezo wa jana wa Ligi Kuu Bara uliokuwa wa kwanza kwake kama kaimu kocha mkuu, Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo, huku akiwapa nafasi Shaaban Idd Chilunda, Moses Phiri, Luis Miquisson, Kennedy Juma na John Bocco walioingoa kipindi cha pili. Phiri ndiye aliyeasisti bao la Jean Baleke lililokuwa la kusawazisha baada ya wageni, Namungo kutangulia kwa bao la Reliants Lusajo.

Sare hiyo imekuja siku chache tangu Simba ilipofumuliwa mabao 5-1 na Yanga kwenye Kariakoo Derby lililopigwa Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuzua sintofahamu klabuni, lakini Cadena amesema ni kweli timu inapitia wakati mgumu, ila sare ya juzi ni mwanzo wa kurejesha furaha kwa mashabiki.

"Ushindani ni mkubwa hakuna timu ya kuidharau katika ligi, kila mchezo nimewaambia wachezaji wangu wapambane kupata matokeo na kuyafanyia kazi aliyowatuma kufanya na nimeanza kupata mwanga, japo ligi inaenda kusimama kupisha mechi za kimataifa," amesema kocha huyo wa zamani wa Azam FC.

Wakati huo huo, mashabiki wa klabu hiyo wamesema viongozi wanatakiwa kuangalia na kujitafakari iwapo wanajiona wameshindwa kuiongoza timu hiyo, waachie ngani ili wakafanye majukumu mengine.

Kelvin Sestus ameliambia Mwanaspoti inaumiza kuona viongozi hao hao ndio waliosajili wachezaji wasiokuwa na ubora wakichukulia jambo la kawaida, wakati mashabiki roho zao zinakuwa juu juu kila timu inapocheza.

"Viongozi wanatakiwa kuwajibika na sio kujifucha kwenye kivuli cha kocha, hata angekuja kocha wa Madrid kwa wachezaji waliopo na ufather waliokuwa nao ni ngumu kutoboa," amesema Kelvin, huku Mariam Hassan ameongeza, wao kama mashabiki wanaumia zaidi kwa kuwa huko mtaani tambo za watani wao ma ikizingatia wanafanya vizuri wanakosa amani hata ya kuongelea mpira.

Shabiki mwingine wa timu hiyo, Frank Mack alisema; "Haiwezekana Uchebe (Patrick Aussems), Kishingo (Sven Vandenbroeck, Pablo (Franco), Mgunda (Juma), Robertinho na wengine wote wasiwe bora na kutimuliwa kila mara! Kuna shida kubwa katika uongozi wetu sema wanajifanya hawaoni, ila wanatakiwa kukaa wakijua Simba ni kubwa kuliko wao walipita wengi sana huko nyuma."

Mack ameongeza kuwa toka ligi imeanza msimu huu wanapata matokeo mazuri, lakini morali za wachezaji zipo chini sana na huenda hii ilichangia kufumuliwa mabao 5-1 na Yanga kikiwa cha kwanza kikubwa tangu walipofungwa mara ya mwisho Juni Mosi, 1968 walipochapwa mabao 5-0 kabla ya Simba kujibu mapigo Julai 19, 1977 kwa kuicharaza mabao 6-0 na kurudia tena Mei 6, 2012 kwa kuikandika tena mabao 5-0.

Katika mchezo huo wa Kariakoo Derby, uliokuwa wa 111 kwa timu hizo kukutana katika Ligi ya Bara tangu 1965, Maxi Nzengeli alifunga mabao mawili, huku Stephane Aziz KI, Kennedy Musonda na Pacome Zouzoua kila mmoja akitupia bao moja, ilihali Kibu Denis aliifunga Simba bao la kufutia machozi.kujibu mapigo Julai 19, 1977 kwa kuicharaza mabao 6-0 na kurudia tena Mei 6, 2012 kwa kuikandika tena mabao 5-0.

Katika mchezo huo wa Kariakoo Derby, uliokuwa wa 111 kwa timu hizo kukutana katika Ligi ya Bara tangu 1965, Maxi Nzengeli alifunga mabao mawili, huku Stephane Aziz KI, Kennedy Musonda na Pacome Zouzoua kila mmoja akitupia bao moja, ilihali Kibu Denis aliifunga Simba bao la kufutia machozi.