Buswita haoni pa kutokea Ligi Kuu

Muktasari:
- Hadi sasa Buswita amefunga mabao matatu huku Namungo ikibakiwa na michezo miwili itakayocheza nyumbani dhidi ya Kagera Sugar (Juni 18, 2025) na KenGold (Juni 22, 2025) kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
KIUNGO wa Namungo FC, Pius Buswita amesema katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizobaki, haoni kama anaweza kuvunja rekodi yake ya mabao saba aliyofunga msimu uliyopita.
Hadi sasa Buswita amefunga mabao matatu huku Namungo ikibakiwa na michezo miwili itakayocheza nyumbani dhidi ya Kagera Sugar (Juni 18, 2025) na KenGold (Juni 22, 2025) kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Buswita alisema msimu huu haukuwa mzuri kwake kwani kuna muda alikaa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
“Kuna kipindi niliumwa hadi nilikwenda kupumzika nyumbani Mwanza baada ya kuona nimezidiwa, ila kwa sasa naendelea vizuri, naamini katika mechi zilizosalia huenda nikafunga mabao ila ngumu kufikisha saba ya msimu uliyopita,” alisema Buswita na kuongeza.
“Mbali na changamoto ya majeraha niliyopitia kwa jumla, msimu ulikuwa mgumu na wachezaji wameonyesha viwango vya juu na vya kuvutia.”
Buswita ambaye aliwahi kuitumikia Mbao, Yanga, Ruvu Shooting na Polisi Tanzania, alisema: “Kwa namna ambavyo msimu huu ulivyo mgumu unatoa picha ya jinsi ambavyo 2025/26 itakuwa ngumu zaidi na kila mchezaji atajipanga kuona huduma yake inakuwa bora.”