Bunda Queens yalamba dili WPL, yatambulisha jezi mpya

Muktasari:
- Bunda Queens itashiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara msimu huu baada ya kupanda daraja msimu uliopita ikiibuka kuwa bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza (WFDL), ambapo itafungua pazia na bingwa mtetezi, JKT Queens Desemba 20 katika Uwanja wa Karume, Musoma
WAKATI joto la Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) likizidi kupanda huku kila timu ikiwa kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya kufungua pazia Desemba 20, Klabu ya Bunda Queens imepata udhamini baada ya kuingia makubaliano ya miaka miwili na kampuni ya ElbeshCare ya jijini Mwanza kwa ajili ya uendeshaji wa timu, kudhamini usafiri na vifaa vya michezo.
Timu hiyo yenye maskani yake wilayani Bunda Mkoa wa Mara ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara, itafungua msimu kwa kuwakaribisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, JKT Queens Desemba 20, mwaka huu katika Uwanja wa Karume, mjini Musoma.
Bunda Queens imeingia makubaliano hayo leo Novemba 30, 2023 jijini Mwanza pamoja na kuzindua jezi mpya zitakazotumika msimu huu, jezi hizo zenye rangi ya kijani (nyumbani), nyeupe (ugenini) na pinki yenye michirizi ya rangi nyeusi ubavuni zitauzwa kwa Sh20,000.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini hapa leo, Mwenyekiti wa Bunda Queens, Stephano Kasonde, amesema mashindano wanayokwenda kushiriki yana mahitaji makubwa ndiyo maana wameamua kuingia makubaliano hayo na kampuni hiyo ya uuzaji na usambazaji wa vifaa tiba ili kusaidia kuwa na uhakika wa kushiriki na kufanya vizuri katika michezo yote bila changamoto.
“Timu imejipanga kuleta ushindani katika ligi ninaomba wapenzi na mashabiki wa Bunda Queens watuunge mkono tumedhamiria hasa kupambana katika soka la wanawake, kuleta ushindani na kuhamasisha na kuibua vipaji vya wasichana katika mkoa wa Mara,”
“Matarajio yetu msimu huu ni makubwa usajili tuliofanya ni mzuri tumefanya maboesho ya kikosi tunawaahidi tutakuwa moja ya timu shindani msimu huu,” amesema Kasonde
Bila kutaja thamani ya mkataba huo, Mkurugenzi wa kampuni ya ElbeshCare, Lugendo Faustine, amesema timu hiyo bado iko katika hali ya kujengwa kwahiyo gharama zake zitaongezeka kadri ya mahitaji hivyo kampuni hiyo imejitolea kuhakikisha inaisaidia.
Amesema katika kuhakikisha inakuwa na uhakika wa kusafiri na kufika kwenye vituo vya mechi, tayari wameagiza basi ambalo litaingia Januari, mwakani huku wakiwa wameshasaini mkataba na kampuni ya usafirishaji kuwahakikisha timu hiyo haikwami kusafiri.
“Kampuni imeamua kwa dhati kuwekeza katika soka la wanawake hasa mkoa wa Mara kutokana na changamoto zilizopo za mila kwahiyo tunaamini katika uwekezaji huu tutaweza kuondoa baadhi ya mila potofu,”
“Tutasaidia timu kufikia malengo yake, tutahusika moja kwa moja katika uendeshaji wa timu ili ifikie malengo yake na kufanya vizuri ili kuinua mpira wa wanawake Kanda ya Ziwa,” amesema Faustine