Bocco kimeeleweka huko

Muktasari:

MASHABIKI wa Simba wala hawana sababu ya kuwa na presha juu ya nahodha wao, John Bocco ‘Adebayor’ kwani kila kitu juu yake Msimbazi kimeeleweka.

MASHABIKI wa Simba wala hawana sababu ya kuwa na presha juu ya nahodha wao, John Bocco ‘Adebayor’ kwani kila kitu juu yake Msimbazi kimeeleweka.

Bocco ni moja ya wachezaji wanaomaliza mikataba ya kuwatumikia mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara mwisho wa msimu huu, lakini Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba, nahodha huyo ana uhakika wa kusalia kikosini baada ya mabosi wa Simba kumalizana na meneja wake.

Mwanaspoti linajua kwamba, meneja wake Jemedari Kazumari aliitwa na Simba na kufanya kikao kizito kisichopungua muda wa saa nne na mmoja wa vigogo wa klabu hiyo kisha wakakubaliana kila kitu.

Mwanaspoti lilimtafuta Kazumari ambaye alikubali kufanya mazungumza ya muda mrefu dhidi ya Simba kuhusu suala la kumuongezea mkataba Bocco.

Kazumari alisema mazungumzo yao yalikuwa ya muda mrefu kutokana na mvutano uliokuwepo wa kimaslahi lakini mwisho wa siku kuna dau ambalo walikubaliana pande zote mbili.

“Tumeshamalizana na viongozi wa Simba kilichobaki ni wao kukubaliana na kutuwekea kile ambacho tulikubaliana ili Bocco aweze kusaini mkataba mpya,” alisema na kuongezea;

“Mazungumzo yetu yalikwenda vizuri ingawa yalikuwa ya muda mrefu ila kikubwa kilichobaki hapa ni Bocco tu kusaini mkataba mwingine mpya na Simba.”

Simba walimsajili Bocco mwaka 2017, kwa mkataba wa miaka miwili uliokuwa na thamani ya Sh30 milioni akitokea Azam kama mchezaji huru ambao ulimalizika mwisho wa msimu wa 2018-19.

Baada ya hapo Bocco aliongeza mkataba mwingine wa miaka miwili ambao ndio unamalizika mwisho wa msimu huu na tayari kila kitu kimekwenda vizuri ili kuongeza mpya.

Msimu huu Bocco licha ya kupata majeruhi pamoja na ushindani ya namba katika kikosi cha Simba anashika nafasi ya pili katika mbio za ufungaji akiwa na mabao tisa mawili nyuma ya kinara, Meddie Kagere mwenye mabao 11.

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Martaza Mangungu alisema suala la mikataba mipya kwa wachezaji wao liko chini ya menejimenti ikiwamo ule wa nahodha wao, Bocco.

“Ni kweli tupo na wachezaji wanaomaliza mkataba, lakini suala lao liko chini ya menejimenti, likikamilika mtajulishwa,” alisema Mangungu.