Bocco, Adam wapewa mchongo Ligi Kuu

Bocco, Adam wapewa mchongo Ligi Kuu

Muktasari:

STRAIKA wa zamani wa Simba na  Mtibwa Sugar, Yusuph Mgwao amesema litakuwa jambo la aibu kuona tuzo ya Mfungaji Bora msimu huu inakwenda kwa wachezaji wa kigeni kitu ambacho amewataka washambuliaji John Bocco, Adam Adam kuhakikisha wanatwaa tuzo hiyo.

STRAIKA wa zamani wa Simba na  Mtibwa Sugar, Yusuph Mgwao amesema litakuwa jambo la aibu kuona tuzo ya Mfungaji Bora msimu huu inakwenda kwa wachezaji wa kigeni kitu ambacho amewataka washambuliaji John Bocco, Adam Adam kuhakikisha wanatwaa tuzo hiyo.

Mpaka sasa Bocco ambaye ni Nahodha wa Simba  anaongoza kwa ufungaji akiwa amepachika bao saba huku Prince Dube wa Azam, Adam Adam (JKT Tanzania) na Meshack Abraham wa Gwambina wakiwa wamefunga mabao sita.

Ndani ya msimu miwili Meddie Kagere  raia wa Rwanda amekuwa akibeba tuzo hiyo ambapo mpaka sasa amefunga mabao manne.

Akizungumza na Mwanaspoti Online leo Ijumaa, Novemba 27, 2020, Mgwao amesema amefurahishwa na kasi ya washambuliaji hao lakini atafurahi zaidi kuona msimu huu tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu inakwenda kwa mshambuliaji mzawa.

“Nimewaona Bocco, Adam wameendelea kuwania nafasi ya ufungaji bora msimu huu nitafurahi sana kuona wanapambana kwa kila mchezo wanaocheza na kufunga mabao ya kutosha ili kukimbizana na akina Dube na Kagere,”

“Unajua ligi ina washambuliaji zaidi ya 50 ambao ni wazawa sasa ni jambo baya kuona tuzo inakwenda kwa straika wa kigeni inabidi wakomae kuhakikisha hii aibu haitokei tena msimu huu,” amesema Mgwao.

Mgwao ambaye kwa sasa anaichezea timu ya Magic Pressure ambao ni mabingwa wa Kombe la FA mkoa wa Singida amesema timu za Ligi Kuu zimeonyesha ushindani mkubwa jambo ambalo kwake limempa nguvu kuona soka la Tanzania linapiga hatua.

“Ligi ina ushindani mkubwa, ni jambo la kujivunia maana kama tukiendelea hivi basi soka letu litafika mbali sana,” anasema straika huyo.

Na MASOUD MASASI